Ajali ya Krismas: Kilimanjaro Express Kulipa Fidia ya Shilingi Milioni 300

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru kampuni ya usafirishaji ya Kilimanjaro Truck Company Limited, kuilipa fidia ya shilingi Milioni 300 kwa familia iliyopoteza mtoto kutokana na ajali iliyosababishwa na moja ya mabasi yake ya Kilimanjaro Express.

Kilimanjaro Trucks Company ndiyo inayomiliki mabasi ya Kilimanjaro Express yanayofanya safari kati ya Arusha, Kilimanjaro na Dar-es-salaam.

Kampuni hiyo sasa inatakiwa kulipa fidia ya Shilingi Milioni 300 za kitanzania kutokana na moja ya mabasi yake kuligonga gari dogo na kusababisha kifo cha msichana.

Gari hilo dogo lilikuwa linatumiwa na familia ya Paul Kisena wakati wakisafiri kutoka Dar-es-salaam kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya, Disemba 2021.

Ajali ilisababisha kifo cha mmoja wa wanafamilia ambaye ni binti mdogo wa Kisena.

Amri hiyo ya mahaka imekuja kutolewa baada ya mwaka mmoja, yaani siku ya Jumatano Desemba 21, 2022.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Leila Mgonya katika hitimisho ya kesi ya madai iliyofunguliwa na mfanyabiashara Leonard Paul Kisena dhidi ya kampuni hiyo.

Kisena aliishitaki Kilimanjaro Trucks Company, Mkurugenzi Mtendaji wake Roland Sawaya ambaye pia ni mmiliki wa kampuni hiyo, pamoja na dereva wa basi lililosababisha ajali, Mjahid Mohamed.

Ajali hiyo ilitokea Desemba 24, 2021 eneo la Kerege wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wakati Kisena alipokuwa akisafiri na familia yake kuelekea kwao Kilimanjaro, akitumia gari lake binafsi.

Katika ajali hiyo, basi la Kilimanjaro aina ya Scania liliacha njia na kuliparamia gari la Kisena aina ya Toyota Landcruiser.

Mtoto wake mmoja wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 16 alifariki dunia.

Kisena mwenyewe pamoja na mkewe na mtoto wao mwingine wa kiume walinisurika japo walipata majeraha.

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari