Wananchi wa wilaya ya Arumeru wanatarajia kuanza kunufaika na huduma za afya kwa ukaribu baada ya benki ya NMB kutoa msaada wa vifaa tiba vya kuanzia katika zahanati ya kikatiti.
Zahanati hiyo ilianza kujengwa 2013 kwa nguvu za wananchi.
Baadae, mwaka 2021 waliongezewa nguvu kwa mchango wa shilingi milioni 10 kutoka kwa Rais Samia Suluhu.
Zahanati hiyo ilikuwa ikikabiliwa na ukosefu wa vifaa tiba ili kuanza huduma za msingi.
“Tulihitaji vifaa vya msingi ikiwemo vipimo vya magonjwa mbali mbali, vitanda vya kulaza wagonjwa, kujifungulia na stendi za drip lakini tunashukuru benki ya NMB tumepeleka maombi kwao na leo wamekuja kutukabidhi” alisema Mganga mkuu wa wilaya ya Arumeru, Maneno Focus.
Alisema kuwa vifaa hivyo vimewapa motisha ya kuanza kutoa huduma katika zahanati hiyo.
Anawaomba pia wadau wengine kujitokeza kuwasaidia kupata vifaa vingine zaidi kama vitanda vya kujifungulia wamama wajawazito, vitanda na magodoro ya kulaza wagonjwa, na vifaa tiba vingine ili kukidhi mahitaji muhimu.
Akizungumzia msaada huo, meneja wa benki ya NMB kanda ya kaskazini, Dismas Prosper alisema kuwa wametoa msaada wa vitanda vya kujifungulia akina mama wajawazito na mizani ya kupimia uzito wa watoto wachanga.
Pia wametoa stendi za dripu, pamoja na vitanda na magodoro ya wagonjwa, sambamba mabati 120 kwa shule ya Sekondari Umoja, vyote hivi vikiwa na thamani ya shilingi milioni saba.
“Msaada huu ni utekelezaji wa vipaumbele vyetu vya kuhudumia jamii hasa kipengele cha Elimu na afya pamoja na majanga endapo yakitokea kutokana na ukweli kwamba maendeleo ya Taifa hutegemea watu wenye afya imara na Elimu bora”
Alisema kuwa msaada huo ni moja ya misaada wanayoendelea kutoa katika jamii nchi nzima kama kurudisha shukrani kwa wananchi ambapo kwa mwaka huu wa 2022 wametenga zaidi ya bilioni mbili.
Nae mkuu wa wilaya wa Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango akipokea vifaa hivyo, aliwashukuru wadau wa maendeleo wote waliosaidia kuongeza nguvu kwa wananchi kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo huku akiwaomba wengine kujitokeza kumalizia vifaa tiba, nyumba za watumishi pamoja na uzio.
“Hizi nguvu zote zina lengo la kuwapatia wananchi huduma bora hivyo nitoe maelekezo kwa maafisa afya na wahudumu wa zahanati hii kuhakikisha mnatoa huduma bora na sio baadae tuje tena hapa kushikana mashati kusuluhisha kesi kati yenu na wagonjwa” alisema Ruyango.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa zahanati hiyo,afisa mtendaji wa Kijiji Cha Kikatiti, Abel Kaaya alisema kuwa mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo, ilianza mwaka 2013 kwa michango ya wananchi na mfuko wa jimbo kiasi cha shilingi milioni 75.
Mwaka 2021 Rais Samia katika ziara yake wilayani Arumeru alichangia shilingi milioni 10 Kwa ajili ya kuendeleza huku halmashauri ya meru ikiongeza milioni 10 na m’bunge milioni tano.
“Wafadhili wengine kutokea Korea walimalizia jengo na kufanya jengo kutumia milioni 128 na kupelewa na vifaa pekee Ili kuanza kabla ya benki ya NMB kuja kutupatia vifaa hivi leo ambavyo vinakwenda kuanzisha rasmi utoaji wa huduma katika zahanati hii”
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo Maria Zakaria alisema kuwa waliamua katika mkutano wa wananchi kuanza ujenzi wa zahanati hiyo baada ya kupitia adha kubwa ya kufuata huduma ya afya mbali na Kwa gharama kubwa huku wanawake wa kujifungua wakipitia Wakati mgumu zaidi kufuata huduma mbali.
Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari