Kassim Mapili: Maisha na Muziki

Kassim Mapili alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu, Tarafa ya Lionya, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937. Hivyo umauti umekuta Mzee Mapili akiwa na umri wa miaka 79.

Alipata elimu ya msingi huko kwao Lipuyu, sambamba na kupata elimu ya dini na mwenyewe aliwahi kusema alianza kupata mapenzi ya kuimba wakati alipokuwa Madrasa akighani Kaswida.

\Mwaka 1958 alijiunga na White Jazz Band iliyokuwa na masikani yake huko Lindi.

Mwaka mmoja baadaye akahamia Mtwara na kujiunga na Mtwara Jazz Band, lakini mwaka 1962 akajiunga na Honolulu Jazz Band ambayo nayo ilikuwa hapo hapo Mtwara.

Mwaka 1963, Mzee Mapili akachukuliwa na TANU Youth League ya mjini Lindi, na kujiunga na bendi ya Jamhuri Jazz Band ya hapo Lindi.

Mwaka 1964 Mzee Mapili akachaguliwa kuanzisha bendi ya TANU Youth League ya Tunduru. Mwaka mmoja baadaye alihamia Kilwa Masoko na kujiunga na Lucky Star Jazz Band ya mji huo.

Baada ya hapo ndipo Kassim Mapili akatua katika jiji la Dar es Salaam na kujiunga na Kilwa Jazz Band iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande.

Kama ilivyokuwa sera ya wakati ule ya kuanzisha vikundi vya sanaa katika sehemu za kazi, majeshi yetu pia yalianzisha bendi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nalo likaanzisha bendi na Mzee Mapili alikuwa mmoja ya waanzilishi wa bendi ya JKT Kimbunga Stereo mwaka 1965.

Polisi nao kama majeshi mengine nayo pia ikaanzisha bendi na Mzee Mapili akajiunga na Police Jazz Band, 15 Desemba 1965. Mzee Mapili ndiye aliyekuwa mwalimu wa bendi ya kwanza ya wanawake nchini Women Jazz Band iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 1965.

Mapili na uanzishwaji wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania..

Mwaka 1982 baada ya semina ya wanamuziki iliyofanyika Bagamoyo, Mzee Mapili alikuwa mmoja wapo wa wanamuziki walioanzisha Chama Cha Muziki wa dansi Tanzania, na akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho.

Akiwa Mwenyekiti wa chama hicho mwaka 1986, aliweza kukusanya kundi la wanamuziki 57 ambao walitengeneza kund lililoitwa Tanzania All Stars.

Kundi hili lilirekodi muziki ambao mpaka leo umekuwa katika kipimo cha juu ambacho hakijafikiwa na wanamuziki wa sasa.

Wakati wa uongozi wa Mzee mapili kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM, Radio Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa, Chama Cha Muziki wa Dansi Tanzania waliweza kufanya tamasha la kushindanisha bendi.

Ni shindalo aina yake na haijawahi kurudiwa tena, shindano hili lililoitwa Top Ten Show lilishirikisha bendi kutoka karibu kila wilaya nchini Tanzania. Uongozi huu aliendelea mpaka mwaka 1990.

Mapili kapitia vikundi vingi vya muziki zikiwemo bendi za Shikamoo Jazz Band, Super Matimila, Gold All Stars na Volcano Stars.

Mwaka 1993 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz Band na katika bendi hii alitunga wimbo wa Eva uliokuwemo katika albamu ya kwanza ya bendi hii.

Alipoacha bendi hii Mzee mapili alipitia Super Matimila, Gold All Stars, na hata kujiunga na binti wa Mbaraka Mwinshehe katika bendi yake ya Volcano Stars.

Katika kipindi cha karibuni alikuwa akishirikiana na Mrisho Mpoto na wasanii mbalimbali katika muziki. Mzee Mapili ameacha watoto watatu.

Tuachie majibu

Anwani yako ya Email haitaonekana