Mashitaka ya kutaka Kulipua Jiji la Dar-es-salaam yaligeuka kuwa Kesi ya Kuipindua Serikali – Lema

Mwanasiasa Maarfu Nchini, Godbless Lema ambaye ndio kwanza amerejea kutoka ughaibuni, anasema kuwa yeye na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe walikuwa wameandaliwa mashitaka ya kutaka kulilipua jiji la Dar-es-salaam.

Anaongza kuwa mashitaka hayo baadae yaligeuzwa kuwa kesi ya Uhaini wakati akiwa Nairobi.

Lema ambaye alikuwa ni Mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka kumi, anelezea kuwa serikali ya Hayati John Pombe Magufuli ilipanga kwamba awekwe kizuizini hadi mwaka 2024 kwa mashitaka hayo, na kwamba mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, viongozi wakuu wa upinzani walianza kukamatwa.

“Mimi na Mwenyekiti wangu, Mbowe tulitoroka nchini, kukimbilia Kenya,” Lema aliuelezea mkutano wa Hadhara jijini Arusha ambako alipokelewa na maelfu ya wanachama wa CHADEMA.

Mwenyekiti wa Chama Hicho, Freeman Mbowe, alikiri kutorokea nchini Kenya, Desemba 2020 baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, John Magufuli mshindi wa kiti cha Urais.

Mapokezi ya Godbless Lema, Arusha

“Lema yeye alipitishwa kihalali katika mpaka wa Namanga lakini mimi ilibidi nitumie njia za panya, ila wote tulikutana Nairobi,” Mbowe anaelezea.

Baadae, akiwa jijini Nairobi, Lema anasema kuwa mashitaka yake huku Tanzania yalibadilishwa yakawa ya Uhaini wa kutaka kuipindua serikali ya Magufuli.

Kutokana na hatua hiyo, Mbunge huyo wa zamani wa Arusha mjini akajua kuwa kifuatacho, iwapo angerudishwa nchini, ni kifo.

Mwingine aliyeikimbia nchi, kuhofia usalama wake, ni aliyekuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye alikwenda mafichoni Ubelgiji.

Godbless Lema, baada ya kupewa hifadhi ya muda nchini Kenya, alikimbilia nchini Canada yeye na mkewe na wanawe watatu.

“Sijarudi na familia yangu kwa sababu nimekuja kwanza kupima hali ilivyo nchini,” Lema anafafanua.

Hata hivyo anaelezea kuwa wakati anatua katika uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, Rais Samia Suluhu Hassan naye alikuwa amefika uwanjani hapo akitokea jijini Dar-es-salaam.

“Nilishangaa sana kusikia Rais Samia aliwasalimia mamia ya wanachama wa vyama vya upinzani waliofika kunipokea KIA,” anasema mbunge huyo wa zamani wa Arusha.

Na alishangaa Zaidi kwamba jeshi la polisi ambalo awali lilikuwa likiwashambulia, sasa limetuma askari kumsindikiza kutoka uwanja wa ndege hadi jijini Arusha na kuulinda mkutano wake wa Mapokezi katika viwanja vya reli.

“Hizi dalili za mwanzo zinaonesha kuwa nchi imebadilika sana kisiasa na kwamba Rais Samia anaunga mkono demokrasia na uhuru wa maoni,” alisema.

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari