TAIFA TANZANIA
Gazeti Huru la Habari za Tanzania, Afrika Mashariki na Zanzibar

Moto walipuka tena Mlima Kilimanjaro

Palipo na Moshi hapakosi Moto na katika wilaya ya Moshi, Moto unaripotiwa kulipuka juu ya Mlima mrefu Barani Afrika. Kilimanjaro.

Moto uliolipuka usiku wa kuamkia Jumamosi ya tarehe 22, Okoba 2022 unaripotiwa kuteketeza maeneo kadhaa ya mlima Kilimanjaro, ambao ndio mrefu zaidi barani Afrika.

Hata hivyo taarifa kutoka uongozi wa Kilimanjaro National Park, Mamlaka inayosimamia mlima huo, zinasema juhudi za kuuzima moto huo tayari zimeanza.

Mioto katika mlima Kilimanjaro imekuwa ni matukio ya kawaida katika miezi ya tisa kumi na kumi na moja, kipindi ambacho hali ya joto huathiri maeneo mengi ya kaskazini mwa Tanzania.

Safari hii moto unaripotiwa kuteketeza maeneo ya juu, katika miinuko ya mlima, usawa wa Mweka.

Hii ni kutokana na taarifa zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Times.

Mwezi na wakati kama huu, mwaka 2020 kuliripotiwa tukio jingine la moto mkubwa katika maeneo kadhaa ya mlima Kilimanjaro.

Moto huo ulianzia maeneo ya Whona na hadi juhudi za kuuzima zilipofanikiwa tayari eneo lenye ukubwa wa kilometa 28 za mraba lilikuwa limeteketezwa.

Baadae, katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, wafanyakazi wanawake kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Ngorongoro na Benki ya CRDB walikwenda kuotesha miche ya miti ya asili kuuzunguka mlima.

Zoezi hilo lilifanyika katika miinuko ya Usseri, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, mwezi Machi, 2021.

Mlima Kilimanjaro, ambao kilele chake cha Kibo ndicho kirefu zaidi, barani Africa, pia ni eneo muhimu ki mazingira, ukiwa ndio chanzo cha maji kwa maeneo mengi Tanzania na Kenya.