TAIFA TANZANIA
Gazeti Huru la Habari za Tanzania, Afrika Mashariki na Zanzibar

Rais wa DR Congo Katika Ziara Tanzania

Rais Tshikedi alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

Kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Felix Antoine Tshikedi yupo nchini Tanzania kwa ziara ya Kikazi.

Tshikedi, ambaye ni Rais wa Tano wa nchi ya DR Congo, awali ikijulikana kama zaire, alitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Julius Nyerere, jijini Dar-es-salaam siku ya Jumapili ya tarehe 23 Octoba, 2022.

Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais Tshikedi alipokelewa na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa serikali ya Tanzania. 

Tshikedi alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kisha kushuhudia ngoma za kitamaduni uwanjani hapo kabla ya kuandamana na mwenyeji wake kuelekea Ikulu ya Dar-es-salaam.

Viongozi hao wawili pia walipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.

DR Kongo ni nchi ya saba kujiunga na Jumuiya ya Afrika mashariki yenye makao yake makuu jijini Arusha, Tanzania.

Congo pia ndio nchi kubwa kuliko zote Afrika Mashariki na Kati, na ya pili kwa ukubwa barani humu baada ya Algeria.

Kongo inapakana na Tanzania kwa upande wa magharibi.

Katika kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na utawala wa kidikteta wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Mobutu Sese Seko, raia wengi wa DRC walikimbilia Tanzania kutafuta hifadhi na wengi kwa sasa wamekuwa ni raia.

Congo pia ni nchi yenye wazungumzaji wengi wa lugha yakiswahili na ni miongoni mwa watumiaji wa bandari ya Dar-es-salaam ingawa wana bandari yao upande wa pili wa bara la Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 2 Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2022.