SERIKALI ya Tanzania imepokea ugeni wa watu 10 kutoka nchini Afrika Kusini waliofika Tanzania kwa lengo la kujifunza juu ya ufugaji nyuki, hasa kwenye maeneo ya uanzishaji wa manzuki na hifadhi za nyuki.
Ugeni huo, uliowasili mapema jana Jijini Dodoma unajumuisha wataalamu na wafugaji nyuki, ambapo malengo yao pia ni pamoja na kujifunza juu ya maandalizi na ukaguzi wa manzuki pamoja na njia bora za kuzuia na kudhibiti wadudu kwenye ufugaji nyuki.
Akiongea mara baada ya wageni hao kuwasili, Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba amesema ziara hiyo ni ya kimkakati na inalenga kuanzisha mazungumzo na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, hususan katika eneo la biashara ya mazao ya nyuki, teknolojia za ufugaji nyuki na utafiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, kutoka Wizara ya Maliasili na Utali, Deusdedith Bwoyo, amesema wageni hao wamehamasika kuja hapa nchini kujifunza namna shughuli za ufugaji nyuki zinavyofanyika.
“Kule Afrika Kusini tumeambiwa wana uwezo wa kuzalisha tani 2000 kwa mwaka wakati asali inayohitajika ni tani 4000 kwa mwaka, Sisi huku tunazalisha tani 32,691 kwa mwaka na asali yote hiyo hutumika kukidhi mahitaji ndani ya nchi kwa takriban asilimia 90 ” amesema Bwoyo.
Pamoja na hayo, Bwoyo ameongeza kuwa, Waafrika Kusini hao wamekuja kujifunza namna bora ambayo itawasaidia kuongeza uzalishaji wa asali nchini kwao, lakini pia, namna ambavyo wanaweza kuwahamasisha watu nchini kwao kutumia asali kwa wingi kama ambavyo zao hilo la nyuki linatumiwa kwa wingi hapa Tanzania
Naye Kiongozi wa Wajumbe hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Zakaria Thupi Mokgathlha, amesema Tanzania ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa kwenye eneo la ufugaji nyuki, hivyo wamekuja kujifunza ili waweze kupata ujuzi utakao wasaidia kujiimarisha kwenye neo hilo.
“ Tumekuja kuangalia Tanzania inavyofanya kwenye eneo hili ili tutakavyorudi kwetu tukaweke mikakati ya kuimarisha sekta hii.” amesema Zakaria.
Katika ziara hiyo, Wataalamu hao watatembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kilichopo mkoani Tabora Uongozi wa Mkoa huo pamoja na Vikundi vya wafuga nyuki vya mkoa huo.
Mara baada ya kuwasili Jijini Dodoma, ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea Ofisi za Manyoni za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) pamoja na Hifadhi ya Nyuki ya Agondi ambapo wamepata elimu ya namna bora ya kufuga na kuchakata mazao ya nyuki hususani asali.