BARAZA la Sanaa la taifa limeanza zoezi la kuwafuata na kuwaibua wasanii chipukizi kokote waliko nchini chini ya programu maalum.
Taarifa kutoka BASATA inaelezea kuwa program hiyi ya mtaa kwa mtaa ina lengo la kuwatambua wasanii wapya, kuwasajili na hata kuwasaidia kukuza vipaji vyao ndani na nje ya nchi.
BASATA imenza utaratibu huu mpya chini ya katibu mtendaji, wa baraza hilo. Kedmond Mapana, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza agizo la Waziri wa Utamaduni Sanaa na michezo Mohamed Mchengerwa.
Inasemekana kuwa Waziri anataka Baraza hilo liwafikie wasanii wote nchini na kuibua vipaji vipya katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Zoezi hilo la mtaa kwa mtaa linatekelezwa kupitia waratibu kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Elizabeth Ncheye pamoja na Agostino Makame.
Akizungumza na gazeti hili mratibu Ncheye alisema wanafanya zoezi na tayari wameanza mkoani Pwani, wilaya ya Rufiji lengo kuu ni kuwafikia wasanii waliopo mtaani ili kukuza na kutambua vipaji vilivyopo.
“Mambo yalikuwa Moto Rufiji ,Utete na ikwiriri kwani wasanii mbalimbali walishiriki katika matukio ya Sanaa zote zilizokuwepo.
Viongozi wa mashirikisho ikiwa ni pamoja na shirikisho la Sanaa za maonesho, ufundi, Muziki na filamu wote wameahidi kuwashika mkono na kuwaendeleza wasanii waliofanya vizuri,”alisema Ncheye.
Alisema pamoja na zoezi hilko la mtaa kwa mtaa, Wizara ya maendeleo ya jamii, wanawake, jinsia na makundi maalumu waliona umuhimu wa Sanaa na kuomba kushirikiana na BASATA kufikisha ujumbe uliopo ‘Sanaa mtaa kwa mtaa,kuza Sanaa tokomeza ukatili.
Utekelezaji wa program ya Sanaa mtaa kwa mtaa utafanyika nchi nzima ambapo umeanza na Rufiji, Pwani lengo ikiwa ni kuibua ,kukuza na kuendeleza vipaji vya Sanaa na awamu itakayofuata itakuwa mkoani Arusha.
Akiwa Rufiji Pwani hivi karibuni Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa alilipongeza BASATA kwa ubunifu waliouanzisha.
Mchengerwa aliwataka wasanii nchini kufanya kazi za Sanaa zenye maudhui ya kupinga ukatili katika jamii na alisisitiza BASATA kuendelea kutekeleza programu za Sanaa kwa watoto kupitia shule za shule za msingi na sekondari ili kupata vipaji .