Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Bei ya Maji Karatu yashuka kwa zaidi ya Asilimia Hamsini

Wakazi wa Karatu mjini mkoani Arusha wameanza kupata maji Safi na salama huduma ambayo imefikia asilimia 73.3 ya upatikanaji.

Awali huduma ya maji mjini Karatu ilikuwa imefikia wananchi kwa asilimia 29.36. Hii ilikuwa ni kabla ya kuunganishwa kwa mamlaka mbili za maji  kuwa chombo kimoja.

Mnamo Agosti Mwaka 2022 Waziri wa maji Juma Aweso aliunganisha kilichokuwa chombo wa watumiaji maji (KAVIWASU) na mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira KARUWASA kuwa chombo kimoja.

Kwa sasa mamlaka jumuishi inajulikana kwa jina la KARUWASA.

Pia kutokana na mabadiliko hayo Bei ya maji ilishuka kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka Shilingi 3000 kwa Unit Moja hadi Shilingi 1300 kwa kipimo hicho.

Waziri alifikia maamuzi hayo kutokana na kilio kutoka kwa wakazi wa mji wa Karatu baada ya Bei hizo kudaiwa kuwa ya juu sana.

Vile vile suala la kuwa na mamlaka mbili za maji ndani ya mji mmoja ni Jambo ambalo wananchi walikuwa wakililalamikia kwa muda mrefu bila mafanikio.

Mji wa Karatu ulikuwa ukihudumiwa na mamlaka hizo mbili huku Kila mamlaka ikiwa na Bei yake ambapo KAVIWASU ilikuwa ikichaji wateja wake shilingi 3000 hadi 3500 kwa unit moja huku mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira KARUWASA ikichaji shilingi 1700kwa unit moja.

Mkurugenzi wa mamlaka ya maji na Safi wa mazingira KARUWASA Steven Siay amesema kuwa baada ya muungano huo mamlaka imeweza kuhudumia wateja wake kwa asilimia hizo tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya taasisi hizo kuungana.

Siay aliyasema hayo wakati akisoma taarifa ya KARUWASA wakati wa makabidhiano ya nyaraka za mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira Karatu, mbele ya timu kutoka wizara ya maji pamoja uongozi wa wilaya

Aidha amefafanua kuwa mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira imeongeza idadi ya wateja katika mji wa Karatu kutoka wateja 1198 hadi  kufikia 4897 baada ya kuundwa mamlaka mpya idadi ambayo inategemewa kupanda kwa asilimia kubwa kutokana na uboreshwaji wa huduma ya maji pamoja na bei kuwa rafiki kwa watumiaji.

Akizungumza na wadau wa maji mgeni rasmi katika makabidhiano hayo mwakilishi wa mkuu wa wilaya ambaye ni katibu tawala wa wilaya Faraja Msigwa alimtaka mkurugenzi waKARUWASA kuhakikisha vyanzo vya maji vinaongezeka ili kufuta changamoto ya uhaba wa maji katika wilaya ya Karatu.