Upungufu wa vifaa vya tiba katika kituo kipya cha afya kitumbaine kilichopo wilayani Longido umekuwa changamoto kubwa kwa wakazi wanaoishi eneo hilo.
Kabla ya serikali kujenga kituo hicho cha afya kwenye kata ya Kitumbeine, wakazi wa vijiji vya eneo hilo walikuwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 60 ili kupata huduma za afya, katika hospitali ya wilaya iliyopo mjini Longido.
Matatizo yalikuwa yakiwaelemea zaidi akina mama wajawazito pamoja na watoto.
“Serikali iliwekeza zaidi ya shilingi milioni 800 katika ujenzi wa kituo cha afya kata ya Kitumbeine,” alisema mganga mkuu wa hosptali ya halmashauri ya Longido Daktari Selemani Mtenjela.
Hata hivyo daktari huyo alibainisha kuwa bado kituo hicho kipya kina upungufu mkubwa wa vifaa vya tiba hususan eneo la upasuaji.
Katika kusaidia kutatua tatizo hilo Benki ya NCBA imetoa msaada wa vifaa vya kufanyia upasuaji kwa wanawake wajawazito katika kituo kidogo cha afya cha kitumbaine kilichopo wilayani Longido.
Vifaa hivyo vimetolewa ili kupunguza changamoto ya huduma kwa mama mjamzito wakati wa kujifungua katika kituo hicho.
Claver Serumaga ambaye ni mkurugenzi mkuu wa benki ya NCBA amesema tumetoa msaada huu kwa kituo cha afya cha kitumbaine ili kusaidia watu wenye uhitaji na pia kuboresha huduma za afya.
Ameongeza kuwa vituo vya afya vina uhitaji mkubwa vya vifaa vya kuwasaidia wagonjwa na huu kwetu sisis ni mwanzo tu wa kutoa msaada bado tunatarajia kufanya mambo mazuri zaidi mbeleni kwa kushirikiana vyema na wadau.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha daktari Sylvia Mamkwe ameishukuru benki ya NCBA na serikali kwa ujumla katika kufanya jitihada za kuboresha huduma za afya.
Amesema tunategemea kuanza kufanya upasuaji katika kituo hicho cha afya baada ya kupokea msaada huo ambao utaenda kutatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Aidha amesema bado kuna upungufu wa vifaa lakini kwa hivi vichache walivyo vipokea vitaenda kutatua changamoto kwa wagonjwa kwani walilazimika kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya lakini hivi sasa hawatalazimika tena kwenda katika hospitali ya halmashauri ya Longido ili kupata huduma.
Wakati huohuo mganga mfawidhi wa kituo cha Kitumbeine Daktari Frank Kimbwereza amesema tumekuwa tukipata changamoto kwa akina mama wajawazito wanaohitaji kufanyiwa upasuaji lakini kupitia msaada huu utaenda kuwa jibu kwa wahitaji wa huduma hiyo.
Aidha amesema kuwa bado tunaendelea kutoa elimu tukishirikiana na viongozi wa kimila kwa akina mama kuja kujifungulia hospitali kwani wengi wao wanajifungulia majumbani kama ilivyozoeleka kwa jamii hiyo.