Tanzania itasamehewa baadhi ya madeni yake ambayo ilikuwa inadaiwa na serikali ya China.
Hili linajitokeza jijini Beijing ambako Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na kiongozi wa China, katika ziara yake ya siku tatu, Mashariki ya Mbali.
Katika safari hiyo ya kikazi Rais Samia Suluhu Hassan pia ameshuhudia utiaji saini wa Mikataba na Hati za Makubaliano ya miradi 15 ya kimkakati.
Kiongozi huyo wa Tanzania pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.
Miongoni mwa mikataba hiyo iliyolenga kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji wa baina ya nchi hizo mbili umeshuhudia China ikiipunguzia Tanzania sehemu ya deni lake la thamani ya Shilingi Bilioni 31.4.
Miongoni mwa mikataba na makubaliano yaliotiwa saini ni kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la usafirishaji wa maparachichi kutoka Tanzania kwenda China.
Pia wametia saini Mkataba unaohusu msaada wa RMB milioni 100 za ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu baina ya nchi hizo mbili.
Vile vile, kumetiwa saini makubaliano kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la Usafirishaji wa Mabondo ya Samaki pamoja na bidhaa nyingine za uvuvi kutoka Tanzania kwenda China.

Aidha, China imetoa mkopo wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 56.72 wenye masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar, Terminal II.
China inaongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania. Hadi kufikia Mwezi Oktoba 2022, Jumla ya miradi 1,098 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 9.6 ilisajiliwa katika kituo cha uwekezaji cha TIC.
Miradi hiyo imezalisha ajira 131,718. Uwekezaji huo umefanyika katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano, madini na uvuvi.
Rais Samia yupo nchini China kwa ziara ya Kiserikali kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa nchi hiyo ambapo pia alikutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa China pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa Xi Jinping alizuru Tanzania mwaka 2013 ikiwa ndio nchi ya kwanza yeye kutembelea mara baada ya kuwa rais.