Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Hifadhi za Taifa Huzungukwa na Vijiji zaidi ya 10,000 katika wilaya 70 za Tanzania Bara

Gari la watalii katika eneo la Kogatende ndani ya hifadhi ya Serengeti wilayani Serengeti mkoani Mara

Huku Tanzania ikiwa na vijiji takriban 12,000 imeelezwa kuwa vijiji vipatavyo 10,000 vilivyopo nchini vimepakana moja kwa moja na hifadhi za taifa.

Hadi sasa nchi ya Tanzania ina jumla ya hifadhi 22 za taifa, yaani National Parks. Idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwemo ndani ya nchi moja duniani.

Ukiongeza na uwepo wa zaidi ya mapori tengefu 40, ni wazi kuwa kila kijiji Tanzania kitakuwa kimepakana na eneo lililohifadhiwa, iwe ni mbuga za wanyama, mapori tengefu, mapori ya akiba au hifadhi za misitu.

Lakini kwa idadi ya hifadhi za taifa ambazo zinazungukwa na vijiji elfu kumi (10,000), zinaelezwa kupatikana katika wilaya zaidi ya 70 nchini nzima.

Kutokana na hali hii, ni wazi kwamba maeneo hayo muhimu ya uhifadhi kwa asilimia kubwa yamo mikononi mwa wananchi wa kawaida walio wengi.

Kwa mujibu Afisa Utalii Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Edmund Murashani, hali hiyo inawafanya mamilioni ya wakazi wa vijiji hivyo kuwa ndio wahifadhi wakubwa na walinzi wa maliasili nchini.

Akizungumza katika kijiji cha Qatesh, wilayani Mbulu, Mkoani Manyara hivi karibuni, Murashani anabainisha kuwa ushirikiano baina ya wananchi, serikali na uongozi wa hifadhi ni muhimu kwa maendeleo ya rasilimali za taifa.

Katika moja ya maeneo ambayo wanavijiji hunufaika na jitihada za uwekezaji ni upande wa huduma za jamii, zikiwemo zile za elimu na afya.

Takriban wakazi 50,000 katika kata ya Gehandu kwenye mji mdogo wa Mbulu, Mkoani Manyara wamejipatia zahanati mpya iliyojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 287 katika kijiji cha Qatesh.

Zahanati hiyo mpya ya Qatesh imejengwa kupitia mradi wa ujirani mwema, katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ambayo iko karibu na maeneo hayo.

Mbali na jingo la matibabu, mradi wa zahanati pia umejumuisha nyumba pacha kwa ajili ya makazi ya madaktari, nyumba hiyo pekee imejengwa kwa thamani shilingi milioni 52.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Sezaria Makota, Hifadhi za Taifa (TANAPA) limechangia Zaidi ya shilingi Milioni 233 huku wakazi wa kijiji cha Qatesh wamechanga milioni 49 huku Halmashauri ya Mji wa Mbulu ikitoa shilingi Milioni 4.4.

“Mradi wa zahanati hasa ni wazo la wananchi na mara baada ya wao kuanza ujenzi ndipo TANAPA wakachangia katika ujenzi,” alisema Mkuu wa Wilaya katika hafla ya makabidhiano ya majengo na vifaa vya tiba.

Kutokana na mafanikio hayo, mkuu wa wilaya ya Mbulu amewasihi wananchi kuendelea kuona umuhimu wa kutunza maeneo ya uhifadhi na kuthamini utalii maana ni chanzo kikuu cha mapato nchini.

“Wakazi wa Qatesh wana sifa moja kubwa nayo ni ile ya ushirikishaji na ndio maana walikuwa wepesi kuleta wazo lao kwetu na sisi tukachangia ujenzi,” anasema Neema Mollel, ambaye ni Mkuu wa hifadhi wa ziwa Manyara.

Kwa mujibu wa Neema, Hifadhi ya Ziwa Manyara pia imejenga choo cha matundu sita kwa ajili ya Zahanati hiyo, kilichogharimu shilingi milioni 15.

“Hata hivyo kwa mwaka wa fedha 2021-2022, hifadhi pia iliomba fedha kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya vifaa vya tiba na tayari  manunuzi yamekwisha kufanyika,” aliongeza mhifadhi huyo.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Peter Sulle ameushukuru uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa kwa kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kupata huduma muhimu ya afya.

Inasemekana kuwa kabla ya Zahanati kujengwa wanavijiji walikuwa wanasafiri umbali mrefu kutafuta huduma za tiba na wakati mwingine akina mama wajawazito walikuwa wanajifungulia njiani.