Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Historia ya Eneo linaloitwa ‘Maji ya Chai’ Arusha

‘Maji ya Chai,’ kwanza ni kijiji. Na kijiji chenyewe kinapatikana kwenye kata inayoitwa ‘Maji ya Chai.’

Kata ya Maji ya Chai ina vijiji vinne ambavyo ni Lerai, Kitefu, Ngurdoto na Maji ya Chai. Kata hii imo ndani ya wilaya ya Arumeru. Jimbo la Arumeru Mashariki.

Zamani enzi za utawala wa wakoloni na mwishoni mwa miaka ya themanini (1980s) eneo la kata ya maji ya chai ilijumlisha na maeneo ya Ngongongare, Ngyeku na Imbaseni.

Eneo lote hilo ilikuwa sehemu maarufu ya malisho ya mifugo ikiitwa Pateny ya Tuvela.

Jina hili Tuvela linatokana na muonekano wa maji yanayopatikana eneo hili.

Sasa watu wanasema kuwa maji ya mto huo yanafanana na chakula maarufu enzi hizo kiitwacho Kivela, ambacho ni chekundu kwa muonekano.

Kivela ni chakula ambacho kinafanana sana na  Kisusio. Ila kivela na kisusio mapishi yake ni tofauti.

Sasa eneo la maji ya chai kuna mto ambao maji yake yana rangi kama chai isiyokuwa na maziwa, au ‘Chai ya Rangi,’ ambayo kule Kenya huitwa ‘Turungi,’ neon lililokokotolewa kutoka maneno ya kiingereza “True Tea” (Chai Halisi).

Maji ya mto huo kufanana na maji ya chai imesababishwa na baadhi ya maeneo ambako maji hupitia yakitiririka kutoka Mlima Meru.

Kuna sehemu ambako maji hukutana na ardhi yenye magadi. Hivyo maji yanapokutana magadi hufanana na maji ya chai.

Kwa sasa jina la asili la eneo hili limebaki kwenye shule ya msingi iitwayo Tuvaila. Vinginevyo hutasikia jina hili likitajwa sehemu nyingine, labda kwenye maharage maarufu yaliyokuwa yakiitwa Ngatuvela.

Kijiji cha maji ya chai kwa upande wa kaskazini kimepakana na kijiji cha Lerai, upande wa mashariki kimepakana na kijiji cha Ngyeku na Kikatiti, kwa uapande wa kusini kimepakana na kijiji cha Kitefu kwa upande magharibi kimepakana na kijiji cha Imbaseni.

Kuna jumla ya  vitongoji  vitatu ambavyo ni  Maji ya Chai Kati, Kimandafu na K/centre. 

Maeneo yaliyokuwa malisho kwa sasa ni makaazi ya watu mfano ulipo Mji Mpya kitongoji cha Maji ya Chai Kati.

Maeneo mengine ya malisho pamejengwa shule ya msingi Maji ya Chai, shule ya sekondari  Maji ya Chai na chuo cha ufundi

Kijiji cha maji ya chai kina shule za msingi za Tuvaila,Kimandafu na Maji ya chai(za serikali) na Sun shield ya binafsi.

Pia kijijini hapa kuna kanisa kongwe la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Maji ya Chai (zamani likiitwa Mura a Munyu).

Kanisa hilo ndilo liliozaa baadhi ya sharika au mitaa kama  Imbaseni na Kikatiti. Ukifika kanisani hapa utakuta kanisa kongwe liliojengwa kwa matofali ya mawe ya kuchonga.

Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa kanisa hilo linaweza kuwa sehemu ya utalii, makumbusho au hata eneo la kuhiji.

Makanisa mengine yaliyopo kijijini ni pamoja na AMEC, Roman Catholic, Seventh Day Adventist na yale ya Pentekoste. Upo pia msikiti mmoja.

Kwa miaka ya karibuni kuanzia 1996 kumekuwa na maendeleo ya kasi sana  kijijini Maji ya chai.

Hospitali ya kisasa ya maji ya chai imejengwa, umeme na maji yapo ya kutosha. Eneo lililokuwa la kulishia mifugo limeugeuka makaazi ya watu kwa kufanyika mji.

Pia kitongoji cha K/Center ambacho ni cha wakulima sasa kuna mabadiliko makubwa kwani sasa ni mji umekuwa kuelekea huku. Viwanja vinauzika kwa kasi sana eneo hili.

Koo zote za vaRwa zinaweza kupatikana katika kijiji hiki kutokana na mwingiliano mkubwa wa kijamii hasa kwenye fursa za kilimo, ujenzi, biashara zinazofanyika kijijini hapa.

Enzi za kabla ya uhuru kulikuwa na akida au Jumbe aliyeitwa Obilio Akyoo ndiye aliyekuwa mtawala na Kiongozi wa eneo hili. Yeye ndiye aligawa bure maeneo kwa wakaazi wa mwanzo wa eneo hili.