Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Kaya zaidi ya 200 zavamia mapito ya wanyamapori Manyara. Ulaji wa Nyama ya Twiga watishia Uhai wa Nembo ya Taifa

Watu wawili Wakazi wa kijiji cha Minjingu, wilaya ya Babati mkoa wa Arusha, Masiali Lais Kipara(19) na Paulo Richard (23) wamekamatwa wakiwa wanamchuna ngozi twiga aliyeuawa hivi karibuni.

Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, George  Katabazi amethitisha kukamatwa kwa watu hao wanaohisiwa kuwa ni majangili.

Tukio hilo ni moja ya madhara yanayotokana na uvamizi wa maeneo ya mapito ya wanyamapori.

Inadaiwa kuwa zaidi ya kaya 200 zimejenga makazi ya kudumu ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja unaoziunganisha hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara.

Uwepo wa makazi na shughuli nyingine za Kibinadamu umeibua sakata jipya la wanyama kuwindwa kwa ajili ya kitoweo na hivi sasa biashara ya Nyama ya Twiga imeshamiri, Babati Vijijini.

Nyama ya Twiga imekuwa ikiuzwa kati ya Shilingi 5000 hadi 10000 kwa kilo.

Kuhusu majangili hao waliokamatwa hivi karibuni, ni katika eneo la jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Burunge (WMA) na askari wa wanyamapori, askari wa Jumuiya ya  hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kwa kushirikiana na Askari wa taasisi ya chem chem ambayo imewekeza katika eneo hilo.

Twiga aliyeuawa alikuwa na  kilo 54.5  mwenye thamani y ash 35.1 milioni na  alikutwa akiwa anachunwa.

Amesema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kwani upelelezi wa shauri lao umekamilika.

Askari wa Wanyamapori ambaye aliongoza operesheni kukamamata watuhumiwa hao, Samweli Bayo,akiwa doria na askari wenzake wa Burunge WMA na Chemchem, alisema waliwakuta watuhumiwa na nyama hiyo, wakijipanga kuanza kuchuna ili wakauze.

Bayo amesema tukio hilo lilitokea February 14, saa 11 jioni na  walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, wakiwa porini na watuhumiwa wengine wawili walikimbia.

Afisa Idaya ya kupambana na ujangili wa taasisi ya Chemchem association ambayo imewekeza Utalii wa picha na hoteli katika eneo hilo, Erick Nyman amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni jitihada za ulinzi shirikishi.

Amesema wamekuwa wakifanya doria  ya pamoja baina ya askari wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA) Askari wa wanyamapori wilaya ya Babati, askari wa Chemchem na askari wa Burunge WMA

Nyman amesema  taasisi hiyo kwa mwaka imekuwa ikitumia zaidi ya sh 400 milioni katika harakati za kupambana na ujangili katika eneo hilo la Burunge WMA  kutokana na kushamiri matukio ya ujangili ukiwepo wa Twiga na wanyama wengine kwa ajili ya kitoweo.

Katika eneo hilo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kumekuwepo na matukio kadhaa ya ujangili wa Twiga na wanyama wengine kwa ajili ya Kitoweo.

Chanzo Cha ujangili kinatajwa na Wananchi kujenga ndani ya maeneo ya mapito ya Wanyamapori na hivyo imekuwa rahisi kuwawinda nyakati jioni.

Hata hivyo tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilianza operesheni ya kupima Ili kutenga maeneo ya mapito ya Wanyamapori katika eneo hilo la Ushoroba wa kwakuchinja