Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Kwanini Nyerere  Aligombana Na Viongozi wa Marekani?

Nyerere akiwa na aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, Jimmy Carter

Hivi ni kwanini hasa Nyerere Alikuwa anatofautiana Na Wamarekani….?

Jibu lake linaandikwa na Maggid Mjengwa kutoka mjini Iringa kama ifuatavyo…

Unabaki kuwa ni ukweli wa kihistoria, kwamba mwaka 1964 ulikuwa ni mwaka mgumu sana kwa uongozi wa Julius Nyerere kuliko wakati mwingine wowote. 

Mwaka huo kulikuwa na matukio makubwa yaliyomtikisa Mwalimu Nyerere pamoja na Tanzania kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Tanzania enzi hizo ikiitwa Tanganyika, lilikuwa bado ni taifa changa.

Sasa baadhi ya matukio ya kipindi hicho cha miaka ya mwanzo ya 60 ni pamoja na Mapinduzi ya Januari 12, visiwani Zanzibar na Uasi wa Jeshi la Tanganyika (Army Mutiny) ulioibuka Januari 20, 1964. 

Matukio yote hayo ya mapinduzi yalijiri ndani ya wiki moja tu.

Ni katika mwaka huo, Wachina na WaCuba waliingia kwa kasi Zanzibar mara baada ya Mapinduzi. Hali hii iliwatisha Wamarekani. 

Haikuishia hapo, ikaja taarifa ya kupandikizwa ya kiintelijensia. Ni katika miezi hiyo hiyo. Kwamba Marekani na Uingereza wanapanga njama za kumwangusha Karume.

Nyerere akaridhia Karume amfukuze Balozi Mdogo wa Marekani kutoka Unguja.

Julius Nyerere akagundua baadae, kuwa alikosea. Akaenda mwenyewe kwa Balozi wa Marekani ili kufafanua kilichotokea. 

Kwenye telegramu ambayo Balozi wa Marekani aliituma White House na shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Januari 1965, Balozi huyo, Bwana Leonhart anauelezea mkutano wake na Julius na kuhitimisha kwa kusema kwamba ”Haukuwa mzuri….”

” Nyerere bekglagade djupt att han kunde inte andra sitt beslut”- (Lugha ya Swedish).

Kwamba Nyerere alisikitika sana lakini hakuwa tayari kubadili uamuzi wake wa Kumfukuza Balozi mdogo wa USA.

(Stig Holmqvist, Pa Vag Mot Presidenten, Ukurasa wa 196). Kimeandikwa kwa lugha ya mwandishi, yaani Kiswidi.

Mengine yaliyojiri kwenye mkutano wa Julius Nyerere na Balozi Leonhart ni vema yakabaki kwenye maandishi ya mwandishi Stig Holmqvist na kwa lugha yake.

Bahati mbaya, kitabu cha Holmqvist hakipatikani kwa lugha ya Kiingereza.

Miaka kadhaa iliyopita nilipata bahati ya kukutana na mwandishi Stig Holmqvist aliyefika Iringa na hata kunitembelea nyumbani. Mwandishi huyo akanipa ruksa ya kukitafsiri kwa Kiswahili kitabu chake hicho. “Ningependa kuifanya, lakini, ni kazi ngumu sana,” nilimjibu.

Hata hivyo, mengine anayosimulia Holmqvist unaweza pia kuyapata kwa lugha ya Kiingereza kwenye vitabu vya waandishi kama vinavyoorodheshwa hapa.

  • The Critical Phase in Tanzania 1945-68: Nyerere and the Emergence of a Socialist Society, Cranford Pratt.
  • Nyerere of Tanzania, William Edgett Smith.
  • The Dark Side Of Nyerere’s Legacy, Ludovick Mwijage).

Hicho kitabu cha Ludovick Mwijage hata hivyo kimepigwa marufuku.