Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Matufaa ya Sodoma sasa yatishia Hifadhi ya Taifa ya Arusha

Vichaka vya mimea vamizi ijulikanayo kama ‘Matufaa ya Sodoma,’ au kwa jina la kienyeji, ‘Ndulele,’ vinachipuka kwa kasi katika hifadhi ya Taifa ya Arusha, ikitishia uoto wa asili pamoja na hatima ya wanyamapori.

Pamoja na Matufaa hayo mwitu, pia kuna mimema mingine vamizi inayojulikana kama miiba ya Morisi ambayo pia inatengeneza vichaka vikubwa vyenye miiba vinavyoziba mapito ya wanyama kuelekea maeneo ya malisho katika hifadhi hiyo ndogo iliyo chini ya Mlima Meru ambao ni wa pili kwa urefu nchini.

Kamishna msaidizi wa uhifadhi, Yustina Kiwango alisema vichaka vya miiba hiyo ya Morisi ijulikananyo kama ‘Mauritius thorns’ na kwa lugha ya kitaalamu ni ‘caesalpia decapilata’ sio tu unaziba njia za wanyama pori na kupunguza maeneo ya malisho, bali kuna uwezekano pia ukawa na madhara mengine kiikolojia.

Mmea mwingine tishio ndio huo ulitajwa awali yaani Matufaa ya Sodoma ambayo ni matunda mwitu yasiyolika na binadamu pamoja na wanyama ambayo kwa kingereza unajulikana kama ‘Sodom Apples’ na kwa kitaalamu ni ‘solanum incanum.’

Katika maeneo mengi ya Tanzania mmea huo ni maarufu kwa jina la Ndulele.

Mhifadhi huyo anabainisha kuwa mimea vamizi inasambaa kwa kasi hifadhini hapo na hadi sasa imefunika asilimia 17 ya eneo zima la hifadhi hali inayoharibu uoto wa asili, kupunguza malisho na kuzuia njia za wanyama.

“Hifadhi nzima ya taifa ya Arusha ina ukubwa wa kilomita za mraba 332,” alisema Kiwango na kuongeza kuwa Mimea hii vamizi imefunika kilomita za mraba 55.

Hifadhi ya Taifa ya Arusha ni maarufu kwa wanyama aina ya twiga, mbega, Tembo, Nyumbu pamoja na misitu asili.

Ndio hifadhi pekee nchini Tanzania iliyowahi kutembelewa na Mfalme Charles III wa Uingereza pamoja na Mkewe, Malikia Mwambata, Camilla.

Hata hivyo kwa mujibu wa kamishna Kiwango, tiyari uongozi wa hifadhi umeanza jitihada za kung’oa mimea hiyo vamizi.

“Sio kazi rahisi na lazima ifanyike kitaalamu ambapo inaweza kuchukua hadi miaka 20 kufanikiwa kuangamiza kabisa mimea hiyo vamizi’

Wakati huo huo watafiti kutoka chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela wanatarahadharisha kuwa kuna mimea mingine vamizi na hatari zaidi aina ya ‘Gugu Karoti,’ inayoinyemelea hifadhi hiyo ingawa bado iko maeneo ya nje.