Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Jitihada zichukuliwe kuzuia milipuko Mingine ya Moto Mlima Kilimanjaro Nyakati za Kiangazi

Taifa Tanzania

Moja ya matukio yaliyotikisa sekta ya uhifadhi mwaka 2022 ni moto uliolipuka usiku wa kuamkia Jumamosi ya tarehe 22, Oktoba.

Moto huo wa mwaka 2022 uliripotiwa kuteketeza maeneo kadhaa ya mlima Kilimanjaro, ambao ndio mrefu zaidi barani Afrika.

Hata hivyo taarifa kutoka uongozi wa Kilimanjaro National Park, Mamlaka inayosimamia mlima huo, baadae zilisema kuwa moto huo ambao mara nyingi hulipuka nyakati za kiangazi kikali, hususan miezi ya Septemba na Oktoba, ulidhibitiwa baada ya kazi nzito ya siku takriban 30.

Mioto katika mlima Kilimanjaro imekuwa ni matukio ya kawaida katika miezi ya tisa kumi na kumi na moja, kipindi ambacho hali ya joto huathiri maeneo mengi ya kaskazini mwa Tanzania.

Safari hii moto uliripotiwa kuteketeza maeneo ya juu, katika miinuko ya mlima, usawa wa Mweka.

Hii ni kutokana na taarifa zilizochapishwa kipindi hicho na gazeti la Tanzania Times. ambalo ndilo lilikuwa la kwanza kabisa kupata taarifa hizo.

Mwezi na wakati kama huo, tena miaka miwili kabla, yaani mwaka 2020 kuliripotiwa tukio jingine la moto mkubwa katika maeneo kadhaa ya mlima Kilimanjaro.

Moto huo ulianzia maeneo ya Whona na hadi juhudi za kuuzima zilipofanikiwa tayari eneo lenye ukubwa wa kilometa 28 za mraba lilikuwa limeteketezwa.

Baadae, katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, wafanyakazi wanawake kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Ngorongoro na Benki ya CRDB walikwenda kuotesha miche ya miti ya asili kuuzunguka mlima.

Zoezi hilo lilifanyika katika miinuko ya Usseri, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, mwezi Machi, 2021.

Mlima Kilimanjaro, ambao kilele chake cha Kibo ndicho kirefu zaidi, barani Africa, pia ni eneo muhimu ki mazingira, ukiwa ndio chanzo cha maji kwa maeneo mengi Tanzania na Kenya.

Sasa wakati hifadhi ya Kilimanjaro inaadhimisha miaka 50 tangu uanzishwa mwaka 1973, moja ya mambo muhimu ya kuzingatia ni kuhakikisha kuwa mara ifikapo kipindi cha kiangazi hatua za awali kudhibiti mioto ambayo pengine inaweza kutokea basi zichukuliwe haraka.