Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mulala: Eneo lililotoa watu Maarufu Meru

Mulala ipo kata ya Songoro wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Kwa upande wa Kaskazini Mulala imepakana na kitongoji cha kisiwani – Kilinga.

Upande wa Kusini, Mulala imepakana na kijiji cha Ngyani. Mashariki Kilinga na magharibi ni kijiji cha Songoro.

Ina vitongoji 4 ambavyo ni Kiuta (Kyuta), Nkoanasari, Nkoatila na Meto.

Wakazi wa Mulala ni wafugaji na wakulima na wao hupenda sana kufuga ng’ombe wa kisasa hasa Friesian na Asian kwa wingi.

Lakini pia wao ni wafugaji wa kuku, mbuzi, kondoo na nguruwe kwa uchache.

Mulala pia ni eneo la mashamba ya mahindi, viazi karoti, maharage,  ndizi, maparachichi, mnafu hasa hasa kitongoji cha Kyuta na pia Kahawa kwa uchache.

Eneo hilo pia imezungukwa na mito miwili mikuu. Mto Mambuku na mtoto Makumira ambayo inatiririsha maji wakati wa Masika tu na muda mrefu inakuwa imekauka.

Koo kubwa zilizopo Mulala ni Nassari, Nnko na Pallangyo. Kuna Koo zingine pia za Meru kwa mfano Mbise, Mafie, Sarakikya na Mungure.

Kama ilivyo katika maeneo mengi ya Meru, wakazi wake wengi ni Wakristo. Hii ni kwa Zaidi ya asilimia 98.

Madhehebu makubwa ni yale ya Kilutheri (KKK) na pia Pentekoste.

Kuna makanisa mawili ya Lutheran, mengine mawili ya FPCT, Moja la EIC, Moja la TAG, Moja la EAGT halafu Victory Church, Lift Him Up na Kanisa la Mungu.

Kuna shule moja ya sekondari ambayo ni ya hivi karibuni, Ilianzishwa mwaka 2021.

Shule ya Msingi pia iko moja nayo ilianzishwa mwaka 1980 na wanafunzi wa kwanza kumaliza hapo ni mwaka 1985 ambapo walihama wakiwa darasa la pili baada ya mgogoro baina ya Mulala na Kilinga kutokea.

Pia kuna shule moja ya English medium ambayo imesajiliwa.

Watu maarufu ni pamoja na Marehemu Eliahu Nassari kati ya wazee wa mwanzo kabisa kuupokea ukristo kupitia KKKT.

Nderingo Pallangyo ambaye ndiye alitoa kiwanja cha kujenga kanisa la kwanza Mulala la kikristo (KKKT). Kabla ya hapo washarika wa mwanzo kutoka Mulala walikuwa wakwenda kuhudhuria ibada eneo la Nkoaranga.

Wengine ni diwani mstaafu Ephata Nnko (Mang’unde), Mkuu wa wilaya ya iramba kwa sasa Mheshimiwa Joshua Nassari na Mkurugenzi wa kituo cha utalii cha Agape Women Group.

Mkurugenzi huyu kimsingi ndiye mwanzilishi wa shule ya sekondari Mulala kwa sababu alifadhili ujenzi wa madarasa manne pamoja na jengo la utawala.

Yumo pia mwanzilishi na mwenyekiti wa kwanza wa kijiji cha Mulala marehemu Eliya leboi ambaye ndiye Baba wa mwalimu Tareto au mwalimu elirehema Nassari.

Mchungaji Estomih Nnko wa kanisa la FPCT Mulala na wengineo.

Familia maarufu Mulala ni pamoja na familia ya kwa mwanuo, (Mwanuo ndiye babu yake askofu Kitoi Nassari, alioa wanawake karibia 60. Ana kijiji chake huko Siha Kinaitwa tindigani).

Wapo pia kina Mawoo, Temba na Lemboto. Bila kumsahau Marehemu Moses Izack Nnko, na askofu Kitoi Nassari.

Vyanzo vikuu vya maji ni Kikororomu na Maambureni vyote kutoka mlima Meru.

Watu wa Mulala wameenea Bateny kuliko vijiji vikongwe vya Varwa. Kata ya Maruvango ni watu kutoka Mulala, nkoasenga na kolila ni watu kutoka Mulala pia.