Umbali wa mita chache tu kutoka lilipo Kanisa la Parokia ya Maguu kuna makaburi mawili yamepakana.
Makaburi hayo ni ya Padre Joseph Damm OSB (1877 – 1956) na kaburi jingine la Mwalimu Christopher Ngong’onda Ngahi.
Ni miaka 67 sasa tangu Padre Joseph Damm OSB alipozikwa katika eneo hilo. Alichagua kuwa azikwe Maguu, Mbinga, badala ya nyumbani kwao Wagenschwend jimbo la Freiburg, Ujerumani.
Aliona vema abaki na Watanganyika (baadae Tanzania) katika ardhi ya Maguu, Mbinga.
Kwa sasa inakaribia karne moja na nusu tangu alipozaliwa.
Joseph Damm alizaliwa tarehe 30 Agosti 1877 huko Wegenschwend jimbo la Freiburg, Ujerumani.
Baada ya kisomo akiwa na umri wa miaka 23 tu alifunga nadhiri akiwa na Shirika la Mtakatifu (Saint) Otillien. Ilikuwa ni tarehe 14 Oktoba 1900.
Ukawa mwanzo wa maisha mapya ya kitume mbali na nyumbani kwao Wagenschwend jimbo la Freiburg, Ujerumani.
Mwaka uliofuatia yaani 1901 alitua katika ardhi ya Wazaramo kwa mara ya kwanza. Naam, aliwasili Dar es Salaam mwaka huo kwa kazi ya utume.
Alipowasili baada ya kupata maelekezo mbalimbali na hali ya maisha ya Dar es Salaam ikiwemo hali ya hewa, alikabidhiwa madaraka ya kusimamia Shule ya Makatekista, Jimbo Katoliki la Dar es Salaam.
Wakati huo Jimbo Katoliki la Dar es Salaam lilikuwa na eneo kubwa la utawala ambapo lilijumuisha maeneo ambayo kwa sasa ni Majimbo ya Dar es Salaam yenyewe, Morogoro, Mahenge, Dodoma, Iringa, Njombe, Songea, Mbinga, Tunduru-Masasi, Lindi na Mtwara.
Wakati huo alikuwa bado hajapata nafasai ya kuwa Padre rasmi. Ilikuwa kama mafunzo kwa vitendo kwake.
Basi mwaka 1903 alirudi jimboni kwake Freiburg, Ujerumani, kukamilisha masomo yake ili awe Padre rasmi.
Aliapishwa rasmi tarehe 23 Julai 1905 kuwa Padre huko Ujerumani. Na mwaka huo huo ndiyo “Jenerali” Kinjeketile Ngwale na jeshi lake aliwavuruga Wajerumani na kuingia kwenye vita vilivyojulikana kama Vita vya Majimaji.
Alitokea kwao Matumbi na kusogea Songea kwa Chifu Mkuu ili kupata baraka.
Kabla ya vita kuanza Kinjeketile alitoweka ghafla na kuonekana siku iliyofuata.
Yeye alieleza kwamba alichukuliwa na mzimu wa vita ili kupata maelekezo ya kupambana na Wajerumani.
Alipoonekana alikuwa amebeba dawa maalum ambayo ikiaminika kuwa na uwezo wa kugeuza risasi kuwa maji; ndiyo ikaitwa Vita vya Majimaji.
Inadaiwa kuwa mtu wa kwanza kuja na dawa iliyoaminika kuwa ni uwezo wa kugeuza risasi kuwa maji ni mpigania uhuru wa Afrika Kusini, bwana Makanda Nxele, zaidi ya miaka 150 iliyopita.
Kinjeketile alitoa kauli kwamba askari wake wasianze kupigana na Wajerumani mpaka atakapotoa ishara fulani ya kuonyesha kuwa sasa waanze pambano. Aliwaasa wakikaidi hili basi wangepigwa vibaya.
Askari wale waliona wanachelewa kuanza mapambano basi wakaingia vitani dhidi ya Wajerumani na ndio walisababisha Kinjeketile akamatwe mapema sana.
Pamoja na kusikia habari za vita kupitia simu ya upepo au “Radio Call” ambayo ilikuwa ni chombo maalum cha mawasiliano kati ya Tanganyika (baadae Tanzania) na Ujerumani, Joseph Damm hakuogopa.
Nia yake ya kurejea Tanganyika ilikuwa bado moyoni mwake. Katika vita hivyo Askofu Kassian Spiss, watawa wawili wa kiume na watatu wa kike waliuawa tarehe 14 Agosti 1905 eneo la Mikukuyumbu. Wengine walikimbia.

Baada ya vita hivyo Joseph Damm alifika tena Tanganyika akiwa padre rasmi.
Alikabidhiwa madaraka ya kusimamia upya na kurejesha shughuli za Parokia ya Lukuledi iliyoharibiwa wakati wa vita.
Alipoona hali njema hapo Lukuledi baada ya kurejeshwa kwa shughuli zake kama kawaida aliwaachia wenzake waongoze, yeye alienda Ulanga ambako akikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Waumini wa dini ya Kiislamu.
Hata hivyo hakutumia mabavu. Kwa maarifa aliyokuwa nayo katika masuala ya Diplomasia aliweza kuishi nao vema kwa amani kisha alianzisha Parokia ya Kiberege.
Baada ya kuona shughuli zinaendelea vizuri katika Parokia ya Kiberege, Joseph alisonga mbele. Alienda kuanzisha Parokia nyingine ambayo ikawa maarufu sana.
Ni Parokia ya Ifakara. Changamoto kubwa ilikuwa Afya. Walipata shida ya mahali pa kupata matibabu endapo wataumwa. Rejea kitabu cha Pugu Hadi Paramiho. Walioanzisha eneo la Pugu walipata shida hiyo pia.
Mwaka 1911 aliondoka Ifakara na kwenda Dodoma. Huko alianzisha Parokia kubwa ya Bihawana.
Alifanya yote haya bila kudai fidia ya kazi hii na hakuna mradi uliokwama. Baada ya kukaa mwaka mmoja kwa mafanikio huko Bihawana alirejea Ifakara.
Mambo yakawa magumu wakati wa vita ya kwanza vya dunia huko Ulaya.
Akiwa na Taifa lililoshindwa vita, Padre Joseph Damm na wenzake walikamatwa na Waingereza kisha wakafanywa kuwa mateka wa vita kisha wakafungwa gerezani huko Misri.
Baada ya mateso ya muda mrefu akiwa mateka wa vita huko Misri waliachiwa huru na walirudi Ujerumani kuanza upya.
Aliporejea Ujerumani alikabidhiwa madaraka ya kuwa mshauri wa kiroho (Spilituare) katika nyumba ya masista wa Tutzing.
Miaka 10 baadae Padre Joseph Damm alirudi tena Tanganyika na kufikia eneo la Lituhi kando ya ziwa Nyasa.
Alitembelea maeneo mbalimbali huko hata katika eneo ambalo mwaka 1932 mabaki ya mjusi mkubwa wa kale yalipatikana.
Eneo la Ngingama, na sampuli za mijusi hao waliitwa Mandasuchus Songeaensis, Nyasasaurus Paringtoni, na Nundasuchus Songeaensis.
Historia ya mijusi ya kale (Dinousarus maarufu kama Dinousar) inatajwa zaidi kutokea msitu wa Amazon nchini Brazil lakini pia katika maeneo ya kando ya mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa palikuwa na mijusi aina hii.
Alielekea katika ardhi ya Wapangwa na kukuta kanisa la UMCA limeanzishwa huko.
Alitafuta eneo jingine na kuanzisha Parokia ya Lugarawa. Wapangwa na Wabena wakawa wanamwita kuwa ni MTUME WA WAPANGWA NA WABENA.
Mwaka 1931 aliondoka Lugarawa na kuwaachia uongozi wenzake aliokuwa nao kisha yeye alitafuta eneo jingine tena. Akapata eneo kwenye ardhi ya Wabena na kuanzisha Parokia ya Uwemba. Kote huko alikopita tangu
Alipoingia nchini kwa mara ya kwanza alisisitiza kuwa na shule kila alikopita ili kuwapa wenyeji fursa ya elimu. Wakaazi wa Uwemba wakawa wanamuita MWAMBA WA UWEMBA.
Hali ya afya yake ilikuwa mbaya lakini alijitahidi sana kuvumilia. Aliona vema maendeleo ya Parokia hiyo kubwa ya Uwemba.
Mwaka 1943 Wamisionari wapya waliletwa ili kumsaidia. Walipofika Uwemba akawakabidhi Parokia hiyo na kuwataka kuisimamia vema na kuhimiza Elimu kwa wenyeji kwa ujenga shule zaidi.
Yeye akaondoka na kwenda eneo jinghyjipya kwake. Na sasa aliwasili katika ardhi ya Wamatengo. Alifika Litembo salama.
Ni Mkoani Ruvuma katika Jimbo Katoliki la Mbinga. Litembo ilikuwa Parokia Kuu ya Wamatengo. Lakini ujio wa Padre Joseph Damm ulibadilisha mambo kwa nia ya njema. Alifanya juhudi kubwa kuipunguzia mzigo Parokia Kuu ya Litembo.
Alijadili na Askofu kisha akamwomba amekabidhi Kigango cha Maguu akiinie kike kuwa Parokia. Kama utani tu, Joseph akaanza kazi ya kuisuka Maguu akiwa na umri wa miaka 66.
Kwa umri huo ilimpasa kupumzika lakini ndiyo kwanza alijiona yungali kijana mwenye nguvu.
Aliona mbele sana kwamba Maguu inaweza kuwa eneo lenye maendeleo. Juhudi za Wabenediktini kutoka Kigonsera mwanzoni mwa miaka ya 1900 katika bonde la Hagati (kuanzia Mikalanga hadi Mkoha) zilimuongoza vema.
Alivutiwa zaidi na kazi za watangulizi wake hasa juhudi za Padre Ludger Brendl kuanzisha Shule (Bush School) Kipapa. Kuanzia mwaka 1914 Maguu ilikuwa sehemu ya Parokia ya Litembo, shule ya awali (Bush School) ilijengwa Mkoha na Kipapa.
Kisha ikahamia Tanga, Makeng’andela na baadae Ndirima. Mapadre watatu waliokuwako Litembo wakati huo ni Padre David Roy, Padre Fulko Schurrer na Padre Leodgar Olbrecht.
Padre Beatus Iten alikuwa Ndirima na alijenga kanisa na shule kwa miti na udongo kisha kuezeka kwa nyasi. Yaani iliwapasa kuanza kutumia malighafi za wenyeji walizozikuta.
Pamoja nao walikuwa Mapadre Einhard Bundschun, Egno Jocher, Innocent Müller, na Halard Jäger ambayo ilikuwa timu iliyofanya kazi ya kuhubiri injili katika bonde la Maguu pamoja na huduma zingine kama elimu na Afya.
Wote hawa waliokuwa Maguu wakiongozwa na Padre Joseph Damm OSB. Chumba chake cha kulala ndicho hicho hicho kilikuwa pia ofisi ya shule. Usafiri wake binafsi ulikuwa ni punda aliyemwita “Rafiki.” Kwa umri wake walimuona kama hangeweza kufanya kazi zaidi.
Na kwamba hana pesa za kuanzisha Parokia na kuiendesha. Hata wenzake walipomuangalia hasa afya yake waliambiana “katika umri huu Joseph, hauna hata senti tano mfukoni, utafaulu kuanzisha Parokia hapa?” Yeye aliona vema kujali nia yake. Hata Wamatengo wenyewe waliona “hiki kizee hakitafanikiwa.”
Mwaka 1947 akawa madhaifu wa afya. Wenzake pamoja na wenyeji waliona wametabiri vema kwamba Joseph Damm hafiki mbali. Lakini waliona wazi pengo atakaloacha.
Alipelekwa Peramiho kwa matibabu, kisha akarudishwa Hospitali ya Litembo. Kwa miezi kadhaa alikuwa hoi bin taabani kitandani akiugua. Hata hivyo kijana mmoja alijitosa katika maombi maalum kwa ajili yake.
Alikuwa ni Bruda Meinrad Eugster kutoka Eunsiedeln nchini Uswisi. Naye alipona vema na kurejea katika kazi za utumishi baada ya wanaume zaidi ya 50 kutoka Maguu kwenda kumchukua kwa machela kutoka Hospitalini Litembo na kumrudisha Maguu, ilikuwa ni tarehe 20 Januari 1948.
Wanaume hao walitembea umbali mrefu walipanda na kushuka milima huku wakiimba. Ni kama safari ya kijeshi inayoambatana na nyimbo za morali.
Hatimaye mwaka 1949 Maguu ilipata hadhi ya kuwa Parokia baada ya juhudi kubwa za Padre Joseph Damm OSB. Yeye akawa Paroko wa kwanza wa Maguu na msaidizi wake Padre Adelgot Ruckli.
Kutokana na changamoto ya makazi ilimpasa Padre Adelgot Ruckli kuishi Mpapa na wakati huo Bruda Gallus na Bruda Gotham walikuwa bize katika eneo la Mtama wakijenga makazi ya Parokia ya Maguu. Mwaka 1952 Maguu ilipata Paroko mwingine Padre Michael Heinlein. Mwaka 1953 Mpapa ikapata hadhi ya kuwa Parokia.
Uongozi wake Padre Joseph Damm OSB ulikuwa wa upendo na kugatua majukumu kama taasisi ndiyo maana kote alikopita kueliendelea bila uwepo wake.
Ikiwa angelikuwa na ubinafsi basi kungekuwa na hali mbaya. Mapadre waliowahi kumhudumia Padre Joseph Damm ni padre Pirmin Freck (1953-1955), na padre Beda Griessl (1955).
November 1955 Padre Lukas Angermaier alifika Maguu kwa kazi ya ujenzi wa Kanisa kubwa, Zahanati na nyumba ya masista.
Padre Joseph Damm alifariki mwaka uliofuata, yaani tarehe 6 Julai 1956 na alizikwa Maguu kama alivyoagiza mwenyewe kwamba asizikwe kwao Wagenschwend jimbo la Freiburg, Ujerumani, bali azikwe Maguu. Alizikwa siku iliyofuata yaani tarehe 7 Julai 1956.
Mapadre wazalendo waliowahi kuhudumia Parokia ya Maguu ni Urban Luambano, Bruno Ndunguru (alikuwa padre wa kwanza mzalendo parokia ya Maguu).
Wengine ni Lukas Komba (Liberatus), Virus Kapinga, Joseph Ngahi, Erasmo Mhagama, Theodus Tulia, Throphor Henjewele, Sales Mapunda, Osmund Nchimbi, Emeran Kihwili, Amon Nchimbi, Alex Nombo, Mose Haule, Erick Kamchatika, na Severine Njako. Wengine ni Paul Chiwangu, Eligius Kapinga, Simon Ndunguru, Joseph Luambano na Kelvin Mbele. Mapadre Wamisionari waliowahi kuhudumia Parokia hiyo ni Beda Ruckli, Guntram Keuling, Hildebrand Meinberg, Andreas Hug, Alfred Müller, Benwad Zöller, na Erich Lammering na wengine zaidi.
Mapadre kutoka Parokia ya Maguu ni Bernard Ndunguru, Maurus Kapinga, Berchmans Ndunguru, Theodos Tilia, Joseph Ngahi, Aidan Nchimbi, Baptist Mapunda, Erich Ndunguru, Ludovick Kapinga, na Jacob Kinunda. Watawa toka Parokia ya Maguu ni Petronilla Ndunguru, Kornelia Hyera, Mpendwa Nombo, Stella Ndunguru, Dhabihu Komba, Luisa Komba, Ines Hyera. Wengine ni Bertha Whero, Renatha Kapinga, Speciola Hili, Bahati Millinga, Janeth Hyera, Gisela Kapinga na wengine zaidi.
Hizo ni juhudi za Padre Joseph Damm OSB pamoja na maneno ya kukatishwa tamaa hakurudi nyuma. Mafanikio yake mengine ni katika Parokia za Bihawana, Lukuledi, Kiberege, Uwemba, Lugarawa na Ifakara. Mateka wa kivita aliyeacha alama kubwa Tanganyika (baadae Tanzania).