Biashara ya kuku mbayo kwa miaka mingi ilikuwa ndio kimbilio la watanzania wengi sasa inakabiliwa na matatizo makubwa ambayo huenda ikaiua kabisa sekta hiyo.
Wafugaji nchini sasa wanaiomba serikali kudhibiti makampuni yanayotoa vifaranga na vyakula vya kuku wa nyama visivyo na ubora kwani vinawadidimiza kiuchumi.
Katika mkutano wao siku moja uliowakutanisha wafanya biashara wa kuku na wafugaji kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga na Dodoma, wafugaji wameonesha kukerwa na makampuni ambayo yanalenga faida badala ya ubora.
Mkutano huo uliofanyika Arusha uliandaliwa na Kampuni ya bidhaa asilia za kuku cha ‘Trow nutrition’
Mmoja wa wafugaji Beatrice Mlay kutoka Moshi anayefuga kuku 500 alisema kuwa ufugaji huo umekuwa na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa ya kuendesha shughuli hiyo.
Wakati huo huobaadhi ya makampuni wakitoa bidhaa zisizo na ubora hali inayowadidimiza kiuchumi.
“Miaka ya nyuma ufugaji ulikuwa unalipa sana kiasi cha kuwa shughuli ya kipaumbele kwa vijana wasio na ajira au wazee wanaostaafu lakini kwa sasa imekuwa inatunyonya hata mitaji yetu kutokana na baadhi ya makampuni kutokuwa waaminifu na bidhaa wanazotuuzia” alisema na kuongeza…
“Tunaomba serikali ifanye msako wa viwanda vya vyakula bubu na wale wanazotengeneza vyakula vizivyo na ubora pia mashamba makubwa ya kuzalisha vifaranga wakaguliwe maana siku hizi vifaranga vingi feki havina ubora vinakufa vikifika bandani na wengine kudumaa bila kukua kwa muda tarajiwa”
Nae Charles Shauri mwenye shamba la kuku 000 alisema kuwa changamoto inayowakabili ni bei kubwa ya vyakula vya kuku wa nyama.
“Bei zimepanda kutoka shilingi 60,000 hadi 65,000 kwa kiroba cha kilo 50 mwaka 2020 hadi bei ya sasa ambayo ni 80,000 hadi 90,000 hali ambayo imepandisha pia bei ya vifaranga kutoka shilingi 1800 hadi 2200 kwa kimoja,” alisema.
” Tatizo hili la chakula kupanda ni bei ya nafaka imekuwa changamoto Sana kiasi cha wafanyabiashara wa chakula kutupandishia bei ya chakula lakini lingine ni ubora wa vyakula vyenyewe viko chini kiasi cha kutulazimu kutumia madawa mengi kutibu kuku na kuwakuza kwa haraka bila kujali afya ya walaji wetu hivyo serikali idhibiti ubora tuwe na amani na kazi hii”
Nae meneja wa kampuni ya bidhaa za kuku kutoka Trouw Nutrition, Joseph Joachim Alisema kuwa wako jijini Arusha kuwapa mafunzo zaidi wafugaji jinsi ya kutumia bidhaa za asili kutoka vya mimea na matunda kukuzia kuku bila madawa yenye kemikali zinazoathiri zaidi walaji wao ambao ni binadamu.
Alisema kuwa changamoto kubwa katika ufugaji ni magonjwa mbali mbali yanayowapata kuku inayotoka na asili ya kifaranga alipototolewa, hali ya hewa, maji na chakula hasa visivyo na virutubisho vya kutosha au vilivyopatwa na ugonjwa sumu kuvu.
“Haya yote yanawalazimu wafugaji kutumia madawa mengi hata yaliyo hatari kwa walaji lakini watatumia kuokoa kuku wao, kutokana na hilo tumekuja na bidhaa kadhaa za kuwasaidia kutibu kifaranga akiwa mdogo, maji ya kunywa lakini pia virutubisho mbali mbali vya chakula Ili kuokoa kuku kudumaa na hizi hazina madhara Wala kemikali”
Alisema kuwa sekta ya ufugaji wa kuku unakua zaidi nchini kutoka kuku milioni 44 kwa miaka mitano iliyopita hadi milioni 92 pamoja na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa wanazokabiliana nazo hasa chakula kuwa ghali na vifaranga huku bei ya kuku ikibakia ndogo hivyo kuiomba serikali kutoa bei elekezi ya vyakula vya kuku na kuku wenyewe sokoni.