Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

‘Sugu’ aapa kumng’oa Spika wa Bunge Jimboni Mbeya

Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina lake la kisanii la ‘Sugu,’ amekamia kumng’oa Spika wa Bunge, Tulia Ackson ambaye kwa sasa ameshikilia Jimbo hilo.

Akizungumza jijini Arusha, katika mkutano wa hadhara wa kumkaribisha aliywkuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Sugu amesema kuwa hata kama uchaguzi ungeitishwa siku inayofuata ana uhakika wa kumshinda Mbunge wa sasa, Tulia Ackson.

“Kwanza akiwa kama spika bunge lake limeshindwa kuwawakilisha wananchi ipasavyo na haliwezi katu kukemea maovu yanayoendelea nchini kama watu kubambikiwa kesi, kufungwa n ahata kuumizwa,” Mbilinyi aliongeza wakati akiwasalimia wananchi wa Arusha.

Tulia Ackson, ambaye awali alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Rais (Magufuli) akiwa Naibu Spika, baadae aligombea ubunge Mbeya Mjini mwaka 2020 na kutangazwa mshindi wa kiti hicho na Tume ya Uchaguzi.

Baadae, aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai alijiuzulu na Tulia Ackson akawa Spika Kamili.

Kwa upande wake, Godbless Lema, ambaye ndio kwanza kawasili nchini akitokea Uhamishoni, Canada amesema Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ameweza kupata nafasi hiyo kwa nguvu za Marehemu, John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Lakini sasa ndio mwisho, mimi ndiye mwenye mji na nimerudi rasmi kuwakilisha vilio vya wananchi!” alisema Lema.

Kwa Mujibu wa Lema, vijana ambao wanadaiwa kujipatia ajira kama waendesha Piki-Piki za Kukodi, yaani Boda-Boda Zaidi wanahatarisha maisha yao kwa kufukuza upepo na kujisababishia magonjwa.

“Ifikie mahali sasa tuyabadilishe maisha ya vijana badala ya kuwahadaa na kuwajaza matumaini ya uongo kwamba kuendesha Boda-Boda kutawatoa kimaisha,” alisisitiza Lema huku akiongeza kuwa mara nyingi umasikini wa vijana ndio umekuwa mtaji wa wanasiasa wengi nchini.

Kuhusu hali ya siasa nchini, Lema anasema dalili za awali zinaonesha mabadiliko makubwa na kurejea kwa demokrasia iliyokuwa imepotea.

Anafafanua kuwa wakati anatua katika uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, Rais Samia Suluhu Hassan naye wakati huo alikuwa amefika uwanjani hapo akitokea jijini Dar-es-salaam.

“Nilishangaa sana kusikia Rais Samia aliwasalimia mamia ya wanachama wa vyama vya upinzani waliokusanyika ili kunipokea pale uwanja wa Kilimanjaro,” anasema mbunge huyo wa zamani wa Arusha.

Na alishangaa Zaidi kwamba jeshi la polisi ambalo awali lilikuwa likiwashambulia, sasa limetuma askari kumsindikiza kutoka uwanja wa ndege hadi jijini Arusha na kuulinda mkutano wake wa Mapokezi katika viwanja vya reli.

“Hizi dalili za mwanzo zinaonesha kuwa nchi imebadilika sana kisiasa na kwamba Rais Samia anaunga mkono demokrasia na uhuru wa maoni,” alisema.