Tanzania inahitaji zaidi ya miche Milioni 50 ya Kahawa, huku uwezo wa taasisi husika ni kuzalisha miche Milioni 20 to kwa mwaka.
Hivyo basi, Taasisi inayojishughulisha na Tafiti za zao la Kahawa nchini, imeanza mkakati wa kuzalisha miche kwa wingi ili kupunguza, kama sio kumaliza kabisa upungufu wa mbegu hizo.
Wataalamu wa TaCRI wanafafanua kuwa ili kuziba pengo lililopo la mahitaji na upatikanaji wa miche ya kahawa miongoni mwa wakulima, ni lazima sasa waweke jitihada za ziada.
“Lengo ni kuboresha zaidi uzalishaji wa zao hili ambalo ni muhimu kiuchumi na biashara hapa nchini.”
Mahitaji ya miche ya kahawa nchini kwa sasa ni kati ya milioni 50 hadi 60 kwa mwaka, lakini uwezo wa Taasisi ya TaCRI ni kuzalisha miche ipatayo milioni 20 tu kwa mwaka.
Hii inaonesha kuwa kuna upungufu wa zaidi ya miche Milioni 30 ya kahawa nchini.
Akiongea wakati wa mahojiano maalumu na Taifa Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa TaCRI, Dokta Deusdedit Kilambo alisema upungufu huo kwa kiasi kikubwa unawafanya wakulima wengi wa kahawa hapa nchini wasifikie uwezo wao kamili wa uzalishaji.
“Tumedhamiria sana kuzalisha miche ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya wakulima katika mikoa yote ambayo zao hilo linastawi, lakini kwa bahati mbaya kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukishindwa kuzalisha miche mingi kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wetu,” alisema.
“Hata hivyo, kwa sasa tunaendesha juhudi na mipango kadhaa ili kuhakikisha tunaanza kuzalisha miche ya kutosha,” alieleza.
Sambamba na hilo, alisema taasisi hiyo yenye makao yake makuu Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro, hadi sasa imefanya utafiti na uzalishaji wa aina zisizopungua 19 za kahawa aina ya Arabika.
Vile vile Tacri imefanya utafiti wa aina nne za Kahawa aina ya Robusta.
Dokta Kilambo ameeleza kuwa aina hizo zina mavuno mengi, na zinastahimili magonjwa makubwa ya kahawa.
“Aina hizi za mbegu ni stahimivu kwa kwa magonjwa ya kawaida ya kahawa ikiwa ni pamoja na Coffee Berry Disease (CBD) na Coffee Leaf Rust (CLR) kwa Arabica na Coffee Wilt Disease (CWD) kwa upande wa kahawa za Robusta. Aina hizi zina sifa zinazokubalika kwa soko la ndani na nje ya nchi,” Dk. Kilambo aliona.
Aidha, alifafanua zaidi kwamba aina hizo zina uwezo wa kutoa kati ya tani mbili hadi sita kwa hekta moja ya kahawa safi (maharage ya kijani kibichi).
“Hata hivyo, angalau aina tatu za kahawa bado ziko mikononi mwa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) zikisubiri kuthibitishwa,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa kahawa ya Tanzania haikabiliwi na changamoto yoyote ya aina bora za kahawa, kwani aina zinazotengenezwa na TaCRI ni miongoni mwa aina bora zaidi duniani.