Tanzania ipo katika mpango maalum wa kuchimba mabwawa zaidi ya 2000 nchini kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kupata maji wakati wote.
Kiongozi wa Ujumbe wa Bunge la Tanzania katika Mkutano wa 53 wa Mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Selemani Jumanne Zedi, amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa kila wilaya nchini inachimbiwa mabwawa 10.
Mradi huo ni maalum kwa ajili ya kukuza sekta ya Kilimo nchini ikiwa ni jitihada za Tanzania kujihakikishia usalama wa chakula.
Zedi alikuwa akiwakilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita cha jukwaa la mabunge ya SADC.
Kiongozi huyo wa Ujumbe kutoka Bunge la Tanzania amesisitiza umuhimu wa nchi za jumuiya hiyo ya maendelo ya kusini mwa Afrika kujitosheleza kwa chakula kupitia kuwekeza katika kilimo chenye tija.
Tanzania bara ina mikoa ipatayo 30 na zaidi ya wilaya 185.
Mradi huo ujulikanao kwa jina la ‘Bwawa la maji kwa Mkulima,’ utawezesha kila wilaya kupata mabwawa 10 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Kwa mara ya nne sasa, nchi ya Tanzania inakuwa mwenyeji wa vikao vya bunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika yaani SADC.
Vikao vya bunge ya 53 vinafanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha chini ya kauli mbiu ya ‘Kilimo cha Kisasa kwa ajili ya kupambana na upungufu wa chakula na kutengeneza ajira kwa vijana.’
Rais Samia Suluhu Hassan aliufungua rasmi mkutano huo ambapo alibainisha kuwa tayari Tanzania imeanzisha mpango maalum wa kuwahusisha vijana katika kilimo cha kisasa.
Vijana wapatao 812 wamechaguliwa kujiunga na Programu hiyo mpya ya Kilimo iitwayo ‘Build a Better Tommorow,’ (Kuijenga Kesho iliyo bora), ambapo watawezeshwa kupata ardhi, mikopo ya fedha pamoja na masoko ya bidhaa zao za kilimo.
Awali Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza katika mkutano huo, alieleza kuwa nchi za Afrika zina zaidi ya Hekari Bilioni 1.2 zinazofaa kwa kilimo lakini maeneo mengi bado hayana umiliki rasmi kwa ajili ya kuyalinda dhidi ya uvamizi na uharibifu.