Akaunti ya Twitter iliyofunguliwa na mtu aitwaye ‘Yesu Kristo,’ na kisha kulipiwa ada ya dola Nane za Kimarekani kwa usajili, imethibitishwa rasmi kule Twitter.
Hatua hiyo imeifanya kampuni ya Twitter kusulubishwa kwa laana kutoka watu mbalimbali wakimlaumu mmiliki mpya wa Twita, Elon Musk kuendekeza pesa zaidi.
Hivi karibuni Musk alitangaza kuwa ili akaunti ya mtu ithibitishwe Twitter, atalazimika kulipia dola nane kila mwezi.
Kutokana na mabadiliko hayo, akaunti za watu wenye uwezo wa kutoa kiasi hicho cha fedha zimekuwa zikipata ithibati kwenye mtandao wa Twitter.
Zaidi ya akaunti Milioni Nane tayari zimethibitishwa baada ya wamiliki wake kulipia ada.
Moja ya akaunti hizo ni ile ya ‘Yesu Kristo,’ ambayo pia imelipiwa.
Kwenye akaunti hiyo ya Twitter, Yesu anajiita ‘Fundi Seremala,’ ‘Mponyaji’ na vilevile ‘Mungu.
Ni ya kiingereza kwa hiyo imeandikwa “Jesus Christ, Carpenter, Healer, God.“
Kuna akaunti nyingi sana za ‘Yesu,’ Twitter lakini hii yenye kishikio cha @jesus ndio imethibitishwa na uongozi wa mtandao huo maarufu kwa habari fupi-fupi.
Akaunti hiyo ya Yesu ambayo inaonesha kuwa ulifunguliwa mwezi Oktoba mwaka 2006.

Wakati inathibitishwa ilikuwa na wafuasi 772,000 lakini hadi sasa ina wafuasi zaidi ya Laki Nane.
Yaani kuna watu 850,000 wanaoifuatilia kwa karibu akaunti ya Yesu, Twitter.
Hata hivyo Yesu mwenyewe, ambaye kaandika kuwa nyumbani kwake ni Israeli, yeye hafuatilii akaunti nyingine yeyote.
Lakini hasa suala la akaunti hiyo kuthibitishwa rasmi na wamiliki wa Twitter ndio limezua tafrani mitandaoni.
Akaunti hiyo tayari ina tiki ya bluu kuonesha kuwa uongozi wa Twitter umethibitisha rasmi kwamba mwenye akaunti hiyo ni Yesu mwenyewe.
Lakini baada ya kupigiwa kelele nyingi, Twitter wamelazimika kufuta tiki ya bluu kutoka kwenye akaunti ya Yesu.
Hata hivyo bado wengine wanahoji kwa nini akaunti nzima isifungiwe maana Twitter walisema wangeziondoa akaunti danganyifu.
Akaunti ya Yesu imeachwa ikiendelea kubandika maandiko kwenye ukurasa wake.
Na ‘Yesu,’ sio mvivu katika ku posti maudhui katika akaunti yake hiyo.
Hata kuna andiko analodai kuwa ‘Ameshauriana na Baba yake (Mungu) kwamba watoto hawatakiwi kupitia aina ya maisha aliyoyapitia yeye akiwa mdogo.’
Katika andiko jingine la mwezi Desemba 2021, ‘Yesu’ wa Twita anadai kuwa baba yake amemuambia kuwa tarehe 25 siyo hasa siku yake ya kuzaliwa lakini haimaanishi kuwa watu waache kufurahia karamu.