Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Vita Vya Uganda havikuibukia Kagera bali Vilianzia Moshi, Kilimanjaro

Mtoto wa Nyerere (Kushoto) na Mtoto wa Idd Amin wakiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro miaka kadhaa iliyopita

Ilikuwa alfajiri, siku ya Jumanne tarehe 31 Octoba 1978, wakati simu ya mezani zilipomzindua Sammy Mdee, aliyekuwa mwandishi wa Mwalimu Nyerere kipindi hicho.

Wito wa simu kwa Mdee ulitoka kwa maripota kadhaa wa vyombo vya kimataifa waliokuwa nchini, wakitaka undani wa taarifa za Radio Tanzania Dar-es-salaam (RTD) zilizodai kuwa Majeshi ya Uganda yamevamia na kumega ardhi ya Tanzania.

Ingawa taarifa za RTD zilikuwa za saa moja asubuhi, Mdee alikuwa bado amelala.

Hii ni kwa sababu usiku ulipita alikuwa amekesha akihangaika na masuala ya Zimbabwe (Rhodesia) na ni hadi saa 11 alfajiri ndipo alipopata nafasi ya kuingia kitandani.

Ukweli ni kwamba siku kadhaa zilizopita majeshi ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin, yalikuwa yamevamia na kumega eneo kubwa la Mkoa wa Kagera.

Kabla ya tukio hilo, inadaiwa vikosi vya ukombozi vya Uganda vilifanya jaribio la kumwangusha mtawala huyo wa mabavu ambaye kila kukicha alikuwa akiendesha mauaji ya kikatili dhidi ya wananchi wake.

Amin alifanikiwa kutoroka kwa kutumia helikopta, huku akiapa kulipiza kisasi kwa Tanzania, nchi ambayo aliituhumu kuhusika.

Wakati huo huo  askari mmoja wa Uganda, aliyekuwa kwenye kambi ya Mutukula, alipenya hadi upande wa Tanzania akiwa na kiu ya bia na baada ya kulewa akasababisha vurugu kubwa zilizopelekea hadi kikosi chake cha jeshi kuingilia kati.

Lakini huku matukio hayo yaliyodaiwa kuchangia vita vya kagera yakifanyika mpakani mwa nchi hizi mbili, mzizi mkuu wa vita baina ya Uganda na Tanzania ulikuwa mbali na hapo.

Mlima Kilimanjaro na Vita vya Uganda

Mwaka 2009, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliwakutanisha pamoja watoto wa waliokuwa Marais wa Tanzania na Uganda, Mwalimu Julius Nyerere na Idd Amin.

Lilikuwa ni tukio la kihistoria, ukizingatia kuwa viongozi hao wawili walidaiwa kuwa mahasimu wakubwa kiasi cha nchi zao mbili kuingia vitani mwezi Novemba mwaka 1978 na kupigana kwa Zaidi ya miezi mitano.

Hiyo ni kabla ya Amin na jeshi lake kuzidiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na yeye kutorokea Libya.

Walioshiriki ni Madaraka Nyerere, mtoto wa Mwalimu, anayeishi kijijini Butiama na Jaffar Remo mtoto wa Amin aliyetokea Dubai wakati huo.

Hawa walikutana mjini Moshi, kabla ya safari ya pamoja kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Jaffar Remo Amin alipopata nafasi ya kuzungumza mjini Moshi, alielezea tukio hilo kuwa kwake yeye suala la kupanda mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika kwa mara ya kwanza, lilimfurahisha sana.

Ila kwa upande wa Madaraka Nyerere, tukio la kupanda mlima Kilimanjaro halikuwa geni kwake; yeye alishawahi kufanya hivyo mara tatu kabla.

Hata hivyo alifurahia kushiriki tukio hilo kwa mara ya nne, ambapo sasa lilikuwa la hisani, kuchangisha fedha kwa ajili ya shule ya wasichana ya Chifu Edward Wanzagi kule Butiama, pamoja na kituo cha kusaidia walemavu na wasiojiweza wilayani Bukoba.

Remo Amin na Madaraka Nyerere walitumia pia safari yao hiyo kumaliza kile kilichoaminika kwa miaka mingi kuwa ni uadui au uhasama baina ya familia hizo mbili za marais wa zamani wa nchi za Uganda na Tanzania.

Kitu ambacho hakikuzungumziwa wakati huo ni kwamba, chini ya Mlima Mrefu wa Kilimanjaro waliokuwa wanaupanda ndipo ulipo mji wa Moshi.

Yoweri Museveni na Mkutano mkuu wa Moshi

Mji wa Moshi ulikuwa na nafasi kubwa sana kwenye vita vya Kagera (1978-1979). Makundi tofauti ya wapiganaji wa zamani wa Uganda dhidi ya utawala wa Amin ndiko walikuwa wameweka kambi zao mjini humo.

Watu wengi wanaamini kuwa vita baina ya Uganda na Tanzania vilianzia Kagera Oktoba 30 mwaka 1978 na kuendelea kwa miezi mitano kabla majeshi ya Tanzania kufanikiwa kumshinda Amin katika wiki ya pili ya mwezi Aprili mwaka 1979.

Idd Amin akiwa na silaha ya kulipua roketi kipindi cha vita mwaka 1979

Lakini wataalamu wa historia wanabainisha kuwa vita kati ya Uganda na Tanzania hasa ilianzia mjini Moshi ambako ndiko makundi ya wapambanaji walikuwa wameweka kambi na ndiko vikosi vilikokuwa vinatokea kwenda kushambulia maeneo kadhaa ya kambi za majeshi ya Amin kuanzia 1972 na kuendelea.

Hii ni baada ya Idd Amin kumpindua aliyekuwa rais wa Uganda, Milton Obote mwaka 1971.

Baada ya tukio hilo, wasomi, wanajeshi na raia wengine wa Uganda zaidi ya 20,000 akiwemo rais wa sasa wa nchi hiyo, Yoweri Kaguta Museveni, walikimbilia Tanzania kuomba hifadhi.

Hata mtoto wa Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alizaliwa nchini Tanzania kipindi hicho.

Katika vipindi na matukio tofauti kati ya mwaka 1972 hadi 1979, vikosi vilivyokuwa Moshi vilikuwa vikiibukia Uganda kwa siri na kufanya mashambulio.

Baadhi ya wapambanaji hao walikamatwa mwaka 1973 na kuuawa kinyama na Idd Amin hadharani.

Katika kitabu chake ‘Sowing the Mustard Seed’ (kuotesha punje ya haradali) Rais Yoweri Museveni anakiri kuwa walianza mashambulizi dhidi ya Amin, Uganda mwaka 1972.

Alibainisha pia kwamba kundi lake la Front for National Salvation (kikosi cha ukombozi wa taifa) lilikuwa limeandaa makambi kadhaa ya wapiganaji nchini humo na yote yakipokea maelekezo kutoka Moshi, Tanzania.

Wakati huo Rais Yoweri Museveni, alikuwa akifanya kazi mkoani Kilimanjaro kama Mwalimu katika Chuo Cha Ushirika Moshi.

Kutokana na mashambulio kadhaa, dhidi yake, Amin alianza kuhisi kwamba kumtuhumu Nyerere ndiye kinara wa hujuma dhidi yake maana wapiganaji waasi wanaopanga kumng’oa walikuwa Tanzania, na hivyo Ikulu ya Dar-es-salaam inahusika na mashambulizi hayo.

Hiyo ilimfanya amchukie sana Baba wa Taifa akimtuhumu kuwa ndiye aliyekuwa anawapa hifadhi, chakula, fedha na silaha maadui zake.

Mbaya zaidi ni kwamba hata Obote Rais aliyepinduliwa na majeshi ya Amin, alikuwa yuko Dar-es-salaam.

Amin ama kwa kupewa taarifa zisizo sahihi kuhusu sehemu gani ‘waasi’ walikuwa wamejificha Tanzania, au kwa ukorofi wake tu, alipanga kuushambulia mji wa Mwanza kwa ndege za kivita.

Hii ni kwa sababu alidhani ndiko mkutano mkuu wa wapinzani wake ndiko ulikoandaliwa.

Lakini hasa mkutano mkuu wa wapinzani wa Amin ulifanyika mjini Moshi.

Kikao hicho kilifanikiwa kuunganisha majeshi na vikundi vyote vya waganda waliokuwa Tanzania wakipanga mashambulizi dhidi ya Idd Amin.

Kikosi cha Kisasi

Vikundi hivyo ni pamoja na ‘Kikosi Maalum,’ kilichoongozwa na Tito Okello, akimshirikisha David Oyite Ojok.

Na pia kundi la FRONASA lililoongozwa na Yoweri Kaguta Museveni, pamoja na kundi lililojulikana kama ‘Save Uganda Movement,’ (Harakati za Kuikomboa Uganda), chini ya Akena P’Ojok, William Omaria na Ateker Ejalu.

Kulikuwa pia kuna ‘Uganda National Movement’ ya akina Edward Rugumayo, Fred Sempebwa, Eriya Kategaya na James Mwebaze.

Halafu ‘Negotiating Committee for Democratic Unity,’ kilichokuwa Dar-es-Salaam kikundwa na Dan Wadada Nabudere; Yash Tandon; Omwony Ojwok na Jack Maumbe.

Pia walikuwepo wanajeshi waliobobea wakiwemo; Kanali Tito Okello; Luteni Kanali Omaria William; Kanali Zede Maruru; Meja Samuel Nanyumba; Oryema Odongkara; Kapteni Captain James Odong; Sajenti Tom Oyo; Sajenti Samuel Okello na Kanali Toko.

Na walijumuishwa pia wale walioitwa watu maalum; Paul Muwanga; na Yusuf Kironde Lule. Kwa pamoja, makundi hayo yaliketi mjini Moshi na kuunda umoja ulioitwa ‘Jeshi la Ukombozi wa Taifa la Uganda (Uganda National Liberation Army) yaani ‘UNLA’.

Umoja huo ndio baadae ulikuja kushiriki bega kwa bega na vikosi vya wapiganaji vilivyoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuikomboa Uganda.