Tuntemeke Sanga mwaka 1995 alikuwa mmoja wa wanachama wa CCM waliotaka kugombea nafasi ya urais baada ya kuchukua fomu kama alivyomwambia Nyerere kuwa azma yake ilikuwa kuliongoza taifa la Tanzania.
Wengine waliochukua fomu mwaka huo ni pamoja na Joseph Warioba, Cleopa Msuya, Horace Kolimba, John Malecela, Jakaya Kikwete, Mark Bomani na Njelu Kasaka.
Alikuwepo pia mgombea pekee mwanamke, Rose Lugendo na Benjamin Mkapa ambaye hasa ndiye aliyefanikiwa kuwa Rais wa awamu ya tatu.
Wananchi walimpenda sana Tuntemeke na alishinda ubunge mara zote kila alipogombea, sababu pia alikuwa na uwezo wa kuongea lugha zote za kusini, yaani kinyakyusa, kihehe, kikinga na kibena kwa umahiri mkubwa.
Alikuwa ana msimamo mkali sana na ni mtu asiyeyumbishwa wala kuogopa kusema kile alichokiamini pia aliheshimiwa na wabunge wenzake, Kila anaposimama akiwa bungeni ili aongee wabunge wengi walikuwa wanarudi ndani ya bunge kumsikiliza.
Alipenda sana kujenga hoja na kumpa wakati mgumu spika wa bunge na alijenga hoja baada ya kufanya utafiti wa jambo analoliongelea.
Kuna siku Tuntemeke alipewa dakika 15 tu na spika wa bunge Pius Msekwa ili aongee lakini akazidisha muda na kutumia nusu saa.
Msekwa alipomtaka akae ,Tuntemeke ambaye alimzidi Pius Msekwa miaka mitano ya umri, alikasirika na kumwambia “Hivi kwenu hakuna wakubwa? Huoni mambo ninayoyaongelea ni muhimu kwa wananchi wetu?
Ukumbi mzima wa bunge uliangua kicheko na hata Mh. Spika mwenyewe aliangua kicheko na baadaye Tuntemeke akakaa chini.
Enzi zile ambazo bunge lilikuwa bado halijajengwa kule Dodoma, vikao vilifanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar-es-salaam.
Tuntemeke siku moja akatinga bungeni suruali yake ya jeans na shati lake la kitenge maofisa wa bunge wakamgomea kuingia ndani sababu vazi alilovaa halikuwa vazi la bunge.
Tuntemeke akaondoka lakini baada ya muda akarudi tena na shati lililoshonwa kiwanda cha Nguo cha Urafiki lakini akiwa amevaa kaptura, walinzi kwa mara nyingine tena wakamzuia lakini hakukubali hivyo ukazuka mtafaruku mkubwa.
Spika kipindi hicho ni Adam Mkwawa ambaye alipoingilia kati Mbunge Sanga alimjia juu na kutaka amuoneshe kifungu cha kanuni alichovunja lakini baadae ikabidi arudi nyumbani.
Tuntemeke enzi zake bungeni alikuwa mtata kweli kweli huku akiwapeleka puta mawaziri na maspika kwa maswali yake na hoja nzito.
Aliporejea kutoka masomoni alianza kufanya biashara, kilimo, sheria na kuingia kwenye ulingo wa siasa ambapo alikwaruzana na Mwalimu Julius Nyerere.
Baada ya kusoma muda mrefu Marekani Sanga aliamini kwamba siasa ya ujamaa na kujitegemea haikuwa na tija na isingeweza kuleta maendeleo.
Kamwe hakuwa akificha msimamo wake huo licha ya kuwa mwanachama wa Tanganyika African National Union (Chama cha TANU) ikiwa chini ya Nyerere mwenye itikadi ya ujamaa.
Alimtaka Rais Julius Nyerere ampishe Ikulu ili ailetee nchi ya Tanzania maendeleo Kwa falsafa ya ubepari na abadili mtazamo wa watanzania wa Tanzania ambao Wengi wao ni wavivu wapendao kujirusha na kuoneana wivu.
Tuntemeke alisema shahada zake saba zilimfanya awe na fikra sahihi za kuleta maendeleo kuliko Mwl Nyerere aliyekuwa na shahada mbili tu na muumini wa ujamaa aliouona unaiharibu nchi.
Suala hilo la Tuntemeke kutaka akae yeye Ikulu halafu Rais aondoke lilimuudhi sana Nyerere akaamua kutumia Sheria yake ya ” The preventive Detention Act 1962″ kumsweka mara moja kizuizini.
Alifungwa kifungo cha nje kijijini kwake Bulongwa ambako aliamuriwa asitoke eneo hilo hadi apate kibali maalum.
Akakaa kizuizini kijiji cha Bulongwa miaka mingi sana na kumsababishia ashindwe kumaliza kozi yake ya PHD ambapo miaka ya baadae alipenda kutania kwa kusema;
“Mimi ni PHD candidate ,nilirudi nchini ili nifanye utafiti kuhusu PHD yangu lakini nikawekwa kizuizini kwa miaka mingi, hivyo nikashindwa kuikamilisha ndio maana najiita ” Dr. Mtahiniwa”.
Siku moja Nyerere alimsamehe Tuntemeke na akaamua kugombea ubunge jimbo la makete mwaka 1980 na kushinda kwa kishindo.
Tuntemeke alianza kupata matatizo ya macho muda mfupi tu kabla ya kuanza kikao cha bunge mwaka 1996 Dodoma, na kupelekwa hospitali ya Muhimbili ambako alilazwa mwezi julai mwaka 1996 ,alipelekwa London ,UK sababu alishapoteza uwezo wake wa kuona kwa asilimia 95 na kufanyiwa operesheni ya macho.
Wizara ya Afya ikamrudisha nchini kwa kudai ilikuwa imemaliza fungu ililotoa kwaajili ya matibabu yake hivyo akalazwa wodi ya mwaisela mwezi Septemba 1996, baada ya kurejea nchini mwezi Agosti 1996 alikuwa hawezi kumtambua mtu kwa kumuona bali kwa sauti yake tu.
Makamu wa Rais Omari Ali Juma na Waziri Mkuu Frederick Sumaye walimtembelea wodini kumjulia hali.
Mwanzoni oktoba 1996 Mh. Tuntemeke akatolewa hospital, katikati ya mwezi juni 1997 alikimbizwa Hospitali ya Aga khan ambako alilazwa ICU kwa wiki mbili na baadae kufariki saa za saba Usiku wa kuamkia Jumatano ya Tarehe 2 Julai 1997 akiwa na miaka 66.
Naibu spika wa bunge Philip Marmo alilitangazia Bunge kesho yake asubuhi kuhusu msiba huo mkubwa na kwamba marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo na moyo pakawa na simanzi sana bungeni.
Jijini Dar es salaam shughuli za mazishi ziliendeshwa na Brigedia Jenerali Peter Ligate na msiba ulikuwa mtaa wa Mansfield kwa mdogo wake Tuntemeke, Alfred Sanga.
Mwili wake ukaagwa Muhimbili jumamosi tarehe 5 Julai 1997 ambapo Rais Mkapa aliongoza mamia ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho ambapo alisema;
“Kifo cha Tuntemeke Sanga kimetuondolea Kiongozi mashuhuri ambaye ametoa mchango mkubwa wa maendeleo ,si tu kwa jimbo la Makete bali nchi nzima kwani alikuwa mzalendo mwenye uchungu na nchi yake, hakuwa Kiongozi mwoga bali alikuwa mkweli daima, Nafasi aliyoiacha itakuwa ngumu sana kujazwa na kwamba mchango wake katika taifa hili utaandikwa katika historia ya nchi yetu”.
Mwili wake ukasafirishwa kwa ndege na kuzikwa Bulongwa jumapili tarehe 6 Julai 1997.
Kabla ya kifo chake Tuntemeke alikuwa ameachana na mkewe Bi Betty Ann Fitzgerald, Mmarekani mweusi aliyezaliwa Marekani mwaka 1939 ,alifunga nae ndoa tarehe 29 Septemba 1964 ,ndoa yao ilikuwa ya kukata na shoka ilifungwa huko kijijni kwake Bulongwa baada ya Tuntemeke kulipa mahali iliyojumuisha ng’ombe ,Kondoo ,mbuzi na kuku.
Hakika ilikuwa harusi ya aina yake ambapo watoto 122 waliovalia mavazi nadhifu waliwarushia maua maharusi hao, waliokuwa wamevaa nguo maridadi za kiafrika zilizotengenezwa nchini Ghana, na kuwaimbia nyimbo kedekede za kikinga na kizungu.
Wazee kwa Vijana kwa wiki nzima walisherehekea ndoa hiyo huku wakila ubwabwa uliopikwa kwenye mapipa 15 na pombe ya ulezi iliyokuwa ya kumwaga, ilikuwa harusi ya Kihistoria ambayo hadi leo haina mfano wake pale Bulongwa.
Aidha harusi hiyo iliweka rekodi ya kuwa harusi ya kwanza Tanzania kuandikwa kwa mapana na marefu kwenye gazeti maarufu la Marekani ” The New York Times la tarehe 1—11—1964″ chini ya kichwa cha habari ” Pittsburgh Girl’s wedding in African Village” .

Tuntemeke alimuona kwa mara ya kwanza Bi Betty alipoenda kutoa mhadhara huko Pittsburgh ,Marekani mwaka 1960 ambako ndio kwao Bi Betty Msomi mwenye shahada ya uzamili, Baada ya uchumba wa miaka minne ,wawili hao ndipo walipooana.
Tuntemeke alizaliwa tarehe 8 Desemba 1930 huko Lupaso kijiji cha Bulongwa ,Njombe ,wazazi wake walikuwa ni watoto wa chifu, watoto wengine wa wazazi hao walikuwa wanaitwa, Rwijiso Anna, Geofrey, na Alfred (Mwenyekiti wa Klabu ya Simba mwaka 1979—-1982).
Alianza shule ya msingi mwaka 1942 huko njombe akiwa na miaka 12 alifanya mtihani wa darasa la nne na kufaulu na hivyo akaendelea ” Middle school ” hadi mwaka 1946 alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi huko na kufaulu.
Akaja kujiunga na sekondari ya Ilboru mwaka 1947 na kumaliza mwaka 1950 ambapo alifaulu vizuri sana ,kidato cha tano na sita alisoma shule ya ” Tabora boys” kuanzia mwaka 1951 hadi 1952.
Baada ya hapo akasoma ualimu kazi iliyokuwa na heshima miaka hiyo baada ya kupata cheti cha ualimu akaenda kufundisha shule ya sekondari ya Ilboru ,akiwa kijana mwenye IQ ya pekee na malengo makubwa alidhamiria Siku moja kusoma fani mbalimbali kwa kadiri itakavyowezekana.
Dhamira hiyo ndiyo iliyomuwezesha kuwa Mtanganyika wa kwanza pekee kupata shahada saba za fani ya biashara ,uhusiano wa kimataifa, utawala, sheria, kilimo, sayansi ya jamii na dini.
Kuhusu dini alizungumza Siku moja bungeni tarehe 24–8—1993 ” nikiwa Marekani nilijifunza na nayajua sana masuala ya dini kwa upande wa wakristo ,waislamu na budha.
Alikuwa pia anafundisha na kutoa mihadhara kwenye Vyuo mbalimbali Nchini humo na alikuwa na uwezo mkubwa wa lugha akiongea kwa ufasaha Kiingereza, kiswahili, kijerumani, na kifaransa.
Mwaka 1962 alianza masomo ya PHD huko “Yale University” PHD hiyo ilihusu maendeleo ya utendaji wa vijijini kozi hiyo ilimpasa kwenda chuo cha Nuffield, UK, na Chuo Kikuu cha DSM.
Alirejea nchini mwanzoni mwa mwaka 1964 akawa Afisa uhusiano wa kampuni ya Riddoch Motors (1964—1965) Aidha kwa mikono yake ,akaijenga nyumba yake kijijni Bulongwa.