Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wizara yataka bodi ya Mikopo kuondoa tatizo la Wanafunzi Kujitoa Masomoni

Wizara ya elimu,Sayansi na Teknolojia imeiagiza bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB) kuboresha huduma ya utoaji wa mikopo ili kuondoa tatizo la baadhi ya wanafunzi kusitisha masomo kutokana na kukosa ada.

Akizungumza leo katika kikao kazi kati ya HESLB, Maofisa kutoka vyuoni na wawakilishi wa wanafunzi chenye lengo la kuweka mikakati ya kuhudumia dawati la wanafunzi ili liweze  kuboreshwa zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa elimu ya juu Evaristo Mtitu amesema uboreshaji wa huduma ya mkopo utasaidia kila mwanafunzi mwenye sifa kuweza kutimiza ndoto yake ya kupata elimu ya juu.

 “Nitoe wito kwa bodi ya mikopo ya elimu ya juu kutumia mafunzo haya kama chachu ya kuleta tija na ufanisi katika upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi,”amesema  Mkurugenzi huyo.

Mtitu amesema serikali wakati wote inaweka mikakati inayosaidia upatikanaji wa fedha za kutosha ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji na wanaotoka kwenye mazingira magumu ya kiuchumi waweze kupata elimu ya juu.

“Na imani yangu wanafunzi wahitaji wa mikopo ya elimu ya juu watapata taarifa za kutosha na kwa wakati namna ya upatikanaji wa mikopo na mahitaji yanayotakiwa wakati wa kuomba mikopo,”amesema Dkt Mtitu.

Pia alisema baada ya mafunzo hayo HESLB ni vyema wakahakikisha walengwa wanapata taarifa stahiki na maelekezo ili wanapoombwa kusiwepo kwa manung’uniko yoyote kwa wanafunzi wenye uhitaji wa mikopo.

Mkurugenzi wa uchambuzi na upangaji wa mikopo kutoka HESLB,Veronica Nyahende amesema kikao kazi hicho kitatoka na maazimio ya uboreshaji wa huduma ya hutoaji mikopo ili kuweza kuwafikia walengwa wanaoshindwa kutekeleza vigezo vya uombaji wa mikopo.

Mmoja wa Ofisa mikopo kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine, Santina Bugenyi amesema changamoto inayowakabili ni baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu kuhairisha masomo kutokana na kukosa fedha ya ada yote hivyo anaiomba bodi hiyo kuweka mazingira ya upatikanaji wa mikopo na utoaji wa taarifa kwa walengwa.

Naye Kamishna wa mikopo wa vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini, Emmanuel Martine anaishukuru serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 573  kwa ajili ya elimu ya juu nchini na inakwenda kinufaisha zaidi ya vijana 640 hivyo ni matarajio yao huduma ya mikopo hiyo itaboreshwa na kuweza kuweka mikakati ya kudumu.