TAIFA TANZANIA
Gazeti Huru la Habari za Tanzania, Afrika Mashariki na Zanzibar

Vifo Zaidi Vyaripotiwa kwenye Ajali ya Ndege Iliyotumbukia Ziwani, Bukoba

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 39 na wafanyakazi wanne, wakiwemo marubani wawili, ilikuwa inatokea jijini Dar-es-salaam, kuelekea Bukoba, ambapo baadae ingekewenda pia jijini Mwanza.

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya shirika la Precision Air, iliyotumbukia ziwani wakati ikijaribu kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba, imefikia 19 sasa.

Awali mganga mkuu wa Mkoa wa Kagera alithibitishwa vifo vya watu watatu ambao miili yao iliopolewa kutoka kwenye ndege iliyozama majini.

Hata hivyo taarifa kutoka idara ya zimamoto na uokozi mkoani Kagera, yenyewe haijataja kwa uhakika idadi kamili ya abiria waliopoteza maisha.

Wakati Jeshi hilo halijui chochote kuhusu waliopona au kufa, mganga mkuu wa mkoa wa Kagera, Issessanda Kaniki amefafanua kuwa awali kulikuwa na marehemu watatu, kati yao wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Baadae waziri mkuu Kassim Majaliwa alithibitisha vifo vya watu 19.

Hata hivyo kazi nzima ya uokoaji imefanywa na wavuvi pamoja na wakazi wa Bukoba.

Janga hilo limetokea wakati ndege aina ya ATR 42-500 ilipoangukia ndani ya ziwa victoria, mkoani Kagera, asubuhi ya Jumapili, Novemba 6.

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 39 na wafanyakazi wanne, wakiwemo marubani wawili, ilikuwa inatokea jijini Dar-es-salaam, kuelekea Bukoba, ambapo baadae ingeondoka tena kuelekea jijini Mwanza, kama isingekuwa ni ajali.

Ndege ya Precision-Air ilikuwa na jumla ya watu 43, wakati inaingia anga la Kagera.

Uwezo wa ndege hiyo aina ya ATR ni kubeba abiria 48, au watu 52 ukiongeza na wahudumu wa ndege.

Tayari 28 wamekwisha kutolewa kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo ya Precision Air (PW).

Na kati ya idadi hiyo ya abiria 28 kuna miili pia ya watu watatu ambao wamekwisha kupoteza maisha.

Baadae miili mingine ilipatikana kutoka kwenye kasha la ndege.

Wakati huo huo ndege husika imeanza kuvutwa kwa kamba ili kuisogeza ufukweni mwa ziwa kwa minajili ya kuwaokoa watu wengine waliobaki humo.

Ndege haikuanguka mbali sana na nchi kavu, kwa hiyo wavuvi waliweza kufika katika eneo la ajali kutumia mitumbwi yao na kuwasaidia wahanga wa ajali hiyo.

Inadaiwa kuwa ndege hiyo ya Precision-Air aina ya ATR 42, kutoka Ufaransa ilinunuliwa mwaka 2010.

Hii ni mara ya kwanza kwa ajali kama hiyo ya ndege kutokea katika ziwa victoria (Nyanza).

Habari zingine zinasema kuwa marubani wa ndege hiyo walijikuta wamenasa kwenye chumba cha kuongozea ndege (Cockpit) baada ya mlango wake kujibana kufuatia ajali hiyo.