Vita kati ya Urusi na Ukraine yatibua Soko la Pilipili Kutoka Tanzania
Bei ya Pilipili Kichaa, moja ya mazao ya shambani ambayo Tanzania imekuwa ikiuza katika masoko ya nchi za nje, inaelezewa kushuka kwa sasa.
Taarifa kutoka TAHA, ambayo ndio asasi kilele inayojishughulisha na masuala ya kilimo na mazao ya maua, mbogamboga, matunda, mimea itokanayo na mizizi na viungo, nchini imetoa taarifa kuhusu mwenendo wa soko la zao la Pilipili Kichaa kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita.
“Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa zao la pilipili kichaa (African Bird Eye Chili) kutokana na fursa kubwa za masoko hasa ya nje,” inasema taarifa hiyo.
“Hata hivyo, mwenendo wa bei ya zao hilo umeshuka kuanzia mwezi Juni mwaka huu hivyo kusababisha wakulima wengi wa pilipili kukosa soko.”
“TAHA ikiwa na jukumu la kufuatilia maendeleo ya tasnia ya kilimo cha mazao ya maua, mboga, viungo na matunda (horticulture) nchini imeona ni vema kutoa taarifa rasmi kuhusiana na changamoto hii pamoja na hatua ambazo tunaendelea kuzichukua tukishirikiana na wadau.”

Inasemekana kuwa Katika kipindi cha mwaka 2020 na 2021, soko la zao la pilipili kichaa lilikua kwa kasi na kuvutia wanunuzi wengi kutoka maeneo tofauti Duniani.
Uhitaji huu katika masoko ya kimataifa ulipelekea wakulima wengi kuhamasika kuingia katika uzalishaji wa zao hili na kuuza kwa makampuni (exporters/off-takers) yanayosafirisha mazao hayo kwenda masoko ya nje.
Miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa zao la pilipili kichaa kutoka Tanzania ni nchi za Hispania na Urusi.
Soko la pilipili sasa limekuwa kichaa
Hata hivyo, vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine iliyoanza mwanzoni mwa mwaka 2022, imesababisha kuvurugika kwa sekta ya usafirishaji na ugavi (logistics and supply chain disruptions) hasa katika Bara la Ulaya.
Kutokana na hali hiyo, wanunuzi wengi wa kimataifa wameshindwa kufikia masoko yao kwa haraka na kwa uhakika, na kupunguza ununuzi wa bidhaa mbalimbali ikiwemo pilipili kichaa.
Taasisi ya TAHA kwa kushirikiana na wadau wengine inasema kuwa sasa imeanza inafanya jitihada za kutafuta masoko mbadala ya Kikanda hususani masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Pia wanasaka fursa kwenye masoko ya pilipili yaliyoko katika nchi za Mashariki ya Kati na Bara la Asia.
Sambamba na jitihada za utafutaji wamasoko mbadala, TAHA inafanya tathmini ya kina katika maeneo yaliyoripotiwa kuwa na changamoto ya soko ili kubaini kiwango cha pilipili kichaa ambazo zimeshavunwa lakini bado hazijanunuliwa na wanunuzi.
Taasisi pia inafanya jitihada za kuwezesha kununuliwa kwa mzigo wote wa pilipili kichaa uliopo kupitia wanunuzi watakaopatikana, pamoja na kuwashauri wakulima kulima mazao mbadala yatakayothibitika kuwa na uhitaji kwenye masoko
Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, inandaa mkutano wa wadau wa zao la pilipili utakaojumuisha wadau wote muhimu kutoka sekta za umma na binafsi ili kujadili mikakati ya kuendeleza zao hili hususan upatikanaji wa masoko, ubora wa mazao, pamoja na uongezaji thamani (Value Addition).
Sambamba na hilo, taasisi inasema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wengine zikiwemo Ofisi za Ubalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali pamoja na Idara ya Masoko katika Wizara ya Kilimo na Taasisi mbalimbali ili kutimiza azma hiyo.
Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari