Vitunguu vya Mang’ola Vyasababisha Machozi Karatu baada ya bei kuporomoka

Vitunguu, Zao kuu la kibiashara wilayani Karatu, linadaiwa kuporomoka kwa kasi baada ya bei ya bidhaa hiyo kuanguka msimu huu.

Kwa miaka mingi zao la vitunguu limekuwa ni dhahabu ambapo gunia moja la mavuno likiuzwa kwa hadi shilingi laki mbili.

Lakini hivi karibuni bei imeporomoka hadi shilingi elfu hamsini tu kwa gunia la kilo 100.

Je nini kimelikumba zao hilo muhimu la biashara kwa wilaya ya Karatu?

Kwa miaka mingi, Wilaya ya Karatu imekuwa ikisafirisha zao la vitunguu vyekundu kwenda kuuza katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudani-Kusini.

Inadaiwa kuwa wafanyabiashara wa Kenya pia hununua vitunguu Karatu kisha kuvifungasha na kuvipeleka nchi za nje.

Wanunuzi pia kutoka nchi jirani nao wamekuwa wakienda moja kwa moja Karatu kwa ajili ya kununua bidhaa hiyo moja kwa moja kutoka kwa wakulima wenyewe.

Karatu ni moja ya halmashauri saba zinazounda mkoa wa Arusha, uliko Kaskazini mwa Tanzania.

Kata ya Mang’ola iliyoko takriban kilometa hamsini kutoka mjini Karatu ndiko yaliko mashamba ya vitunguu.

Ni safari ya saa mbili kutoka stendi kuu ya mabasi Arusha hadi mjini Karatu kwa usafiri wa umma.

Ni mwendo wa kilometa 130 kutoka Arusha hadi Karatu mjini.

Usafiri ni pamoja na mabasi makubwa, ambayo hupatikana zaidi muda wa mchana, lakini kuna magari madogo aina ya Toyota Noah ambazo zinakuwepo nyakati zote.

Kutoka karatu hadi Mang’ola ni takriban kilometa 60 ambazo zote ni kupitia barabara ya vumbi yenye mashimo mengi kuelekea Ziwa Eyasi.

Kipindi cha mvua, huwa ni matope na korongo.

Usafiri kwenda mangola zaidi ni kwa magari aina ya Landrover na Landcruiser yenye uwezo wa kuhimili njia mbovu za porini.

Safari kutoka Karatu hadi Mang’ola ni kupita kwenye uwanda mpana wenye miti michache, ardhi kavu ya udongo mwekundu na kama ni mchana, jua kali kuanzia asubuhi.

Ila unapoingia Mang’ola ghafla hali ya nchi inabadilika na kuwa ya kijani kibichi.

Kijani hicho sio cha uoto wa asili, hapo tayari umekwisha fika eneo la kilimo cha vitunguu vyekundu vya Mang’ola.

Wazalishaji wa vitunguu wa eneo hilo huendesha kilimo hicho kupitia skimu ya Umwagiliaji.

Kuna zaidi ya Hekta 5600 za mashamba ya vitunguu kwenye kata ya Mang’ola, wilayani Karatu.

Kuna wakulima wapatao 17,000 wanaojishughulisha na zao la vitungu vyekundu.

Lakini kwa nini hasa kilimo hiki kifanyike eneo la Mang’ola tu, ambako hakufikiki kirahisi, wakati kuna maeneo mengi ya kilimo wilayani Karatu?

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Karatu, Ibrahim Nyigo anafafanua;

“Hiki ni kilimo cha umwagiliaji, na hili eneo la Mang’ola limo ndani ya bonde la Ziwa Eyasi ambalo huwa na maji mengi kutoka milimani,” anaeleza.

Vile vile udongo wa Mang’ola ni wa asili wenye rutuba inayochangia kukoleza ladha na ule wekundu wa vitunguu.

Vitunguu vya Mang’ola vinajulikana kimataifa kama ‘Red Creole Onions,’ kutokana na rangi yake nyekundu inayong’aa.

Aina hii ya vitunguu vya asili hupendwa sana duniani kote.

Na vitunguu vya Karatu vimekuwa na soko kubwa Afrika hasa kwa sababu ni mbegu asili, yenye ladha halisi na ule ukali wa vitunguu.

Sasa ni kwa nini ghafla bei ya bidhaa hii imeanza kuporomoka?

“Sababu kubwa ni kwamba, wateja wetu wakubwa ni wafanyabiashara kutoka nchini Kenya ambao kwa kipindi hiki cha uchaguzi nchini mwao, kidogo wamepunguza sana safari za kuja kununua bidhaa Tanzania,” anafafanua Zaidi Afisa Kilimo wa Karatu, Ibrahim Nyigo.

Kwa mujibu wa Nyigo, msimu huu pia ni wa mavuno kwa zao la vitunguu katika baadhi ya maeneo ya kule Kenya na pia mkoani Kilimanjaro, hivyo basi wateja wao kwa sasa wamepata sehemu nyingine za kupata bidhaa hiyo.

Msimu wa mavuno ya vitunguu sehemu nyingi Kenya huwa kati ya mwezi wa Nane hadi wa Kumi, hivyo wanunuzi wa huko watapungua sana kipindi hiki.

“Bei ya vitunguu imeporomoka sana, maana awali tulikuwa tunauza gunia moja kwa kati ya shilingi 180,000 na 200,000 kutegemea na mteja lakini Sasa imeshuka hadi shilingi 50,000 kwa gunia moja,” alisema Joseph Chuwa mkulima wa Mang’ola.

Wateja wengi wa vitunguu kutoka Karatu wanapatikana katika miji ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Kaskazini Mashariki mwa Kenya, mpakani na Somalia.

“Kipindi cha masika kitunguu kilikuwa juu na wateja walipanga foleni kusubiri lakini Sasa wengi waliotesha na wamevuna, Serikali itusaidie kupata teknolojia ya kuongezea thamani vitunguu vyetu tufungashe na kusafirisha nje kama wenzetu wa Kenya wanavyofanya”

Mkuu wa wilaya ya Karatu Dadi Kolimba alisema Serikali imeanza mchakato wa kutafuta soko la moja kwa moja la zao hilo kuliko kutegemea wateja wa nje.

“Tumeanza kwa kujenga soko letu wenyewe kubwa ambalo wateja watalazimika kwenda hapo kununua na sio kufika shambani kuwalangua wakulima,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

“Lakini pia nitumie nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji kuja Karatu kuwekeza kwenye kilimo hiki cha vitunguu na kuongeza nguvu ya upatikanaji wa zao hilo kwa uhakika,” aliongeza Kolimba.

Mkuu huyo wa wilaya anasema kuwa bado kuna maeneo mengi yaliyo wazi ambayo yanafaa kwa kilimo cha vitunguu, katika kata ya Mang’ola.

Zaidi ya kutumika kama chakula au viungo vya vyakula, Vitunguu pia hutumika kutengeneza aina mbalimbali za dawa za tiba za magonjwa ya ngozi, maumivu ya mishipa na mifumo ya hewa.

Pia hutumika kutengeneza bidhaa za vipodozi.

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari